Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 16:11-23

1 Samweli 16:11-23 SRUV

Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hadi atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na Roho ya BWANA ikamjia Daudi kwa nguvu kuanzia siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama. Basi, Roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mniletee. Ndipo mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mtoto mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yuko pamoja naye. Basi Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese akasema, Mtume Daudi mwanao kwangu, aliye pamoja na kondoo. Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akawa mtu wa kumchukulia silaha zake. Kisha Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu. Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjia Sauli, ndipo Daudi alipokishika kinubi na kukipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.