1 Samweli 16
16
Samweli ampaka Daudi mafuta
1Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli hadi lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.”
2Lakini Samweli akasema, “Nitaendaje? Sauli atasikia kuhusu jambo hili na ataniua.”
Mwenyezi Mungu akamwambia, “Chukua ndama jike, useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.’ 3Mwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakalofanya. Utanipakia mafuta yule nitakuonesha.”
4Samweli akafanya kile Mwenyezi Mungu alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?”
5Samweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu.
6Walipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu anasimama hapa mbele za Mwenyezi Mungu.”
7Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. Mwenyezi Mungu hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini Mwenyezi Mungu hutazama moyoni.”
8Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu Mwenyezi Mungu hakumchagua.” 9Kisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu Mwenyezi Mungu hakumchagua.” 10Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “Mwenyezi Mungu hajawachagua hawa.” 11Hivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?”
Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.”
Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi hadi afike.”
12Basi akatuma aitwe, naye akaletwa. Aling’aa kwa afya, na mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza.
Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Inuka na umpake mafuta; huyu ndiye.”
13Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumpaka mafuta mbele ya ndugu zake. Kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama.
Daudi katika utumishi kwa Sauli
14Basi Roho wa Mwenyezi Mungu alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu ili imtese.
15Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho mbaya imeachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu nayo inakutesa. 16Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walio hapa watafute mtu anayeweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.”
17Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.”
18Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. Mwenyezi Mungu yu pamoja naye.”
19Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” 20Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe.
21Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake. 22Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.”
23Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli 16: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.