Soma Biblia Kila Siku Oktoba/2022Mfano
Akaongozwa na Roho (m.1). Haikutokea kwa bahati mbaya bali ilikuwa ni mpango wa Mungu. Yesu ni Adamu wa pili. Katika 1 Kor 15:21-22 na 45 tunasoma hivi: Kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Na kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Alikuja ili ayatengeneze yale yaliyoharibika kwa kuanguka kwa Adamu. Paulo anaeleza kuwa, kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki (Rum 5:19). Ilibidi ajaribiwe na Ibilisi kama Adamu ili amshinde: Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi (1 Yoh 3:8). Kweli Yesu alimshinda, maana alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda (m.13). Tena baada ya kufufuka, Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani (Mt 28:18)! Alimshinda Ibilisi kwa niaba ya wanadamu wote. Kwa hiyo ukijaribiwa na Ibilisi usiogope bali umshinde kwa kuliitia jina la Mshindi, jina la Yesu. Ahadi ya Mungu ni kwamba kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka (Rum 10:13)! Pia tumia upanga wa Roho ambao ni Neno la Mungu (Efe 6:17)!
Andiko
Kuhusu Mpango huu
Soma Biblia Kila Siku Oktoba/2022 ni mpango wa kusoma Biblia sehemu kwa sehemu kila siku kwa mwezi wa Oktoba pamoja na maelezo mafupi yatakayokusaidia kuelewa kwa urahisi na kuendelea kutafakari neno la Mungu ulilosoma kwa siku husika. Katika mpango huu utasoma zaidi katika kitabu cha Luka. Karibu kujiunga na mpango huu na usome bure
More
http://www.somabiblia.or.tz