Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 94:1-23

Zaburi 94:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwenye kulipiza kisasi, ewe Mungu mlipiza kisasi, ujitokeze! Usimame, ee hakimu wa watu wote; uwaadhibu wenye kiburi wanavyostahili! Waovu wataona fahari hata lini? Watajisifia mpaka lini, ee Mwenyezi-Mungu? Hata lini waovu watajigamba kwa maneno? Waovu wote watajivuna mpaka lini? Wanawaangamiza watu wako, ee Mwenyezi-Mungu, wanawakandamiza hao walio mali yako. Wanawaua wajane na wageni; wanawachinja yatima! Wanasema: “Mwenyezi-Mungu haoni, Mungu wa Yakobo hajui!” Enyi wajinga wa mwisho, fikirini kidogo! Enyi wapumbavu, mtapata lini maarifa? Aliyefanya sikio, je, hawezi kusikia? Aliyeumba jicho, je, hawezi kuona? Mwenye kutawala mataifa, je, hawezi kuadhibu? Mkufunzi wa wanadamu, je, hana maarifa? Mwenyezi-Mungu ayajua mawazo ya watu; anajua kwamba hayafai kitu. Heri mtu unayemfunza nidhamu, ee Mwenyezi-Mungu, mtu unayemfundisha sheria yako, ili siku ya taabu apate utulivu, hadi waovu wachimbiwe shimo. Mwenyezi-Mungu hatawaacha watu wake; hatawatupa hao walio mali yake. Maana hukumu zitatolewa kwa haki tena, na wanyofu wote wa moyo wataizingatia. Nani aliyenisaidia kumpinga mtu mwovu? Nani aliyekuwa upande wangu dhidi ya wabaya? Mwenyezi-Mungu asingalinisaidia, ningalikwisha kwenda kwenye nchi ya wafu. Nilipohisi kwamba ninateleza, fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zilinitegemeza. Mahangaiko ya moyo wangu yanapozidi, wewe wanifariji na kunifurahisha. Wewe huwezi kushirikiana na mahakimu dhalimu, wanaotunga kanuni za kutetea maovu. Wao wanaafikiana kuwaangamiza waadilifu, na kuwahukumu watu wasio na hatia wauawe. Lakini Mwenyezi-Mungu ni ngome yangu; Mungu wangu ni mwamba wa usalama wangu. Uovu wao atawarudishia wao wenyewe, atawafutilia mbali kwa sababu ya ubaya wao. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, atawafutilia mbali!

Shirikisha
Soma Zaburi 94

Zaburi 94:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ee BWANA, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze, Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. BWANA, hadi lini wasio haki, Hadi lini wasio haki watashangilia? Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi? Ee BWANA, wanawaponda watu wako; Wanautesa urithi wako; Wanamwua mjane na mgeni; Wanawaua yatima. Nao husema, BWANA haoni; Mungu wa Yakobo hatambui. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? Aliyelitia sikio mahali pake, asisikie? Aliyelifanya jicho, asione? Awaadibuye mataifa, asikemee? Amfundishaye mwanadamu, asijue? BWANA anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili. Ee BWANA, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako; Ukimponya katika siku za shida, Hadi asiye haki atakapochimbiwa shimo. Kwa kuwa BWANA hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake, Maana hukumu itarejea kwa wenye haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? Kama BWANA asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya. Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee BWANA, fadhili zako zilinitegemeza. Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zinaifurahisha roho yangu. Je! Watawala waovu wanaweza kushirikiana nawe, Wale watungao madhara kwa njia ya sheria? Kwa pamoja wanaishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia. Lakini BWANA amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, BWANA, Mungu wetu, atawaangamiza.

Shirikisha
Soma Zaburi 94

Zaburi 94:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ee BWANA, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze, Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. BWANA, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia? Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi? Ee BWANA, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako; Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima. Nao husema, BWANA haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione? Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue? BWANA anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili. Ee BWANA, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako; Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo. Kwa kuwa BWANA hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake, Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? Kama BWANA asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya. Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee BWANA, fadhili zako zilinitegemeza. Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu. Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria? Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia. Lakini BWANA amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, BWANA, Mungu wetu, atawaangamiza.

Shirikisha
Soma Zaburi 94

Zaburi 94:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ee BWANA, ulipizaye kisasi, Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa. Ee Mhukumu wa dunia, inuka, uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili. Hata lini, waovu, Ee BWANA, hata lini waovu watashangilia? Wanamimina maneno ya kiburi, watenda mabaya wote wamejaa majivuno. Ee BWANA, wanawaponda watu wako, wanawaonea urithi wako. Wanamchinja mjane na mgeni, na kuwaua yatima. Nao husema, “BWANA haoni, Mungu wa Yakobo hafahamu.” Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu; enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima? Je, aliyeweka sikio asisikie? Aliyeumba jicho asione? Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu? Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa? BWANA anajua mawazo ya mwanadamu; anajua kwamba ni ubatili. Ee BWANA, heri mtu anayeadhibishwa na wewe, mtu unayemfundisha kwa sheria yako, unampa utulivu siku za shida, mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya mwovu. Kwa kuwa BWANA hatawakataa watu wake, hatauacha urithi wake. Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki, wote walio na mioyo minyofu wataifuata. Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu? Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu? Kama BWANA asingelinisaidia upesi, ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo. Niliposema, “Mguu wangu unateleza,” Ee BWANA, upendo wako ulinishikilia. Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu, faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu. Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe, ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake? Huungana kuwashambulia wenye haki, kuwahukumu kufa wasio na hatia. Lakini BWANA amekuwa ngome yangu, na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia. Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao; BWANA Mungu wetu atawaangamiza.

Shirikisha
Soma Zaburi 94

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha