Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 94

94
Mungu hakimu wa wote
1Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwenye kulipiza kisasi,
ewe Mungu mlipiza kisasi, ujitokeze!
2Usimame, ee hakimu wa watu wote;
uwaadhibu wenye kiburi wanavyostahili!
3Waovu wataona fahari hata lini?
Watajisifia mpaka lini, ee Mwenyezi-Mungu?
4Hata lini waovu watajigamba kwa maneno?
Waovu wote watajivuna mpaka lini?
5Wanawaangamiza watu wako, ee Mwenyezi-Mungu,
wanawakandamiza hao walio mali yako.
6Wanawaua wajane na wageni;
wanawachinja yatima!
7Wanasema: “Mwenyezi-Mungu haoni,
Mungu wa Yakobo hajui!”
8Enyi wajinga wa mwisho, fikirini kidogo!
Enyi wapumbavu, mtapata lini maarifa?
9Aliyefanya sikio, je, hawezi kusikia?
Aliyeumba jicho, je, hawezi kuona?
10Mwenye kutawala mataifa, je, hawezi kuadhibu?
Mkufunzi wa wanadamu, je, hana maarifa?
11 # Taz 1Kor 3:20 Mwenyezi-Mungu ayajua mawazo ya watu;
anajua kwamba hayafai kitu.
12Heri mtu unayemfunza nidhamu, ee Mwenyezi-Mungu,
mtu unayemfundisha sheria yako,
13ili siku ya taabu apate utulivu,
hadi waovu wachimbiwe shimo.
14Mwenyezi-Mungu hatawaacha watu wake;
hatawatupa hao walio mali yake.
15Maana hukumu zitatolewa kwa haki tena,
na wanyofu wote wa moyo wataizingatia.
16Nani aliyenisaidia kumpinga mtu mwovu?
Nani aliyekuwa upande wangu dhidi ya wabaya?
17Mwenyezi-Mungu asingalinisaidia,
ningalikwisha kwenda kwenye nchi ya wafu.#94:17 nchi ya wafu: Au nchi ya kimya.
18Nilipohisi kwamba ninateleza,
fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zilinitegemeza.
19Mahangaiko ya moyo wangu yanapozidi,
wewe wanifariji na kunifurahisha.
20Wewe huwezi kushirikiana na mahakimu dhalimu,
wanaotunga kanuni za kutetea maovu.
21Wao wanaafikiana kuwaangamiza waadilifu,
na kuwahukumu watu wasio na hatia wauawe.
22Lakini Mwenyezi-Mungu ni ngome yangu;
Mungu wangu ni mwamba wa usalama wangu.
23Uovu wao atawarudishia wao wenyewe,
atawafutilia mbali kwa sababu ya ubaya wao.
Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, atawafutilia mbali!

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 94: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia