Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 94:1-23

Zaburi 94:1-23 SRUV

Ee BWANA, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze, Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. BWANA, hadi lini wasio haki, Hadi lini wasio haki watashangilia? Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi? Ee BWANA, wanawaponda watu wako; Wanautesa urithi wako; Wanamwua mjane na mgeni; Wanawaua yatima. Nao husema, BWANA haoni; Mungu wa Yakobo hatambui. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? Aliyelitia sikio mahali pake, asisikie? Aliyelifanya jicho, asione? Awaadibuye mataifa, asikemee? Amfundishaye mwanadamu, asijue? BWANA anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili. Ee BWANA, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako; Ukimponya katika siku za shida, Hadi asiye haki atakapochimbiwa shimo. Kwa kuwa BWANA hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake, Maana hukumu itarejea kwa wenye haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? Kama BWANA asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya. Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee BWANA, fadhili zako zilinitegemeza. Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zinaifurahisha roho yangu. Je! Watawala waovu wanaweza kushirikiana nawe, Wale watungao madhara kwa njia ya sheria? Kwa pamoja wanaishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia. Lakini BWANA amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, BWANA, Mungu wetu, atawaangamiza.

Soma Zaburi 94