Hesabu 27:1-11
Hesabu 27:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirza walikuwa binti zake Selofehadi. Naye Selofehadi alikuwa mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase mwanawe Yosefu. Basi, hao binti wanne walimwendea Mose, wakasimama mbele yake na kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya ya Waisraeli, kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasema, “Baba yetu alifia jangwani nyikani na bila mtoto yeyote wa kiume. Yeye hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora waliokusanyika dhidi ya Mwenyezi-Mungu, bali alikufa kutokana na dhambi yake mwenyewe. Kwa nini basi jina la baba yetu lifutwe katika ukoo wake kwa sababu hakuwa na mtoto wa kiume? Tupe urithi pamoja na ndugu zake baba yetu.” Mose akaleta lalamiko lao mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wanachosema binti za Selofehadi ni kweli; wape urithi pamoja na ndugu za baba yao, wachukue urithi wake. Kisha waambie Waisraeli kwamba mtu yeyote akifa bila kuacha mtoto wa kiume, urithi wake atapewa binti yake. Ikiwa hana binti, basi urithi huo watapewa ndugu zake wa kiume. Na ikiwa hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utawaendea baba zake, wakubwa na wadogo. Na ikiwa baba yake hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utakuwa wa jamaa yake wa karibu, naye ataumiliki kama mali yake. Hii itakuwa kanuni na sheria kwa Waisraeli, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyokuamuru.”
Hesabu 27:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati huo wakakaribia hao binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya; Mala, na Nuhu, na Hogla, na Milka, na Tirza. Nao wakasimama mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema, Baba yetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha BWANA katika mkutano wa Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume. Kwa nini basi jina la baba yetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake baba yetu. Basi Musa akaleta neno lao mbele ya BWANA BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Hao binti za Selofehadi wananena lililo haki; kweli utawapa milki ya urithi pamoja na ndugu za baba yao; nawe utawapa urithi wa baba yao. Kisha utanena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtu akifa, naye hana mwana wa kiume, ndipo binti yake atapewa urithi wake. Tena ikiwa hana binti, mtawapa nduguze urithi wake. Na ikiwa hana ndugu, mtawapa ndugu za babaye huo urithi wake. Tena ikiwa babaye hana ndugu, utampa huyo aliye karibu naye katika jamaa zake huo urithi wake, naye atakuwa nao; na neno hili litakuwa ni amri ya hukumu kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa.
Hesabu 27:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati huo wakakaribia hao binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa. Nao wakasimama mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema, Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha BWANA katika mkutano wa Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume. Kwa nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu. Basi Musa akaleta neno lao mbele ya BWANA BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Hao binti za Selofehadi wananena lililo haki; kweli utawapa milki ya urithi pamoja na ndugu za baba yao; nawe utawapa urithi wa baba yao. Kisha utanena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtu akifa, naye hana mwana wa kiume, ndipo utampa binti yake urithi wake. Tena ikiwa hana binti, mtawapa nduguze urithi wake. Na ikiwa hana ndugu, mtawapa ndugu za babaye huo urithi wake. Tena ikiwa babaye hana ndugu, utampa huyo aliye karibu naye katika jamaa zake huo urithi wake, naye atakuwa nao; na neno hili litakuwa ni amri ya hukumu kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa.
Hesabu 27:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Binti za Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, walikuwa wa koo za Manase mwana wa Yosefu. Majina ya hao binti yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Walikaribia ingilio la Hema la Kukutania na kusimama mbele ya Mose, kuhani Eleazari, viongozi na kusanyiko lote, wakasema, “Baba yetu alikufa jangwani. Hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora, ambao walifungamana pamoja dhidi ya BWANA, lakini alikufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe na hakuacha wana. Kwa nini jina la baba yetu lifutike kutoka ukoo wake kwa sababu hakuwa na mwana? Tupatie milki miongoni mwa ndugu za baba yetu.” Kwa hiyo Mose akalileta shauri lao mbele za BWANA, naye BWANA akamwambia Mose, “Wanachosema binti za Selofehadi ni sawa. Ni lazima kwa hakika uwape milki kama urithi miongoni mwa ndugu za baba yao, na kubadili urithi wa baba yao uwe wao. “Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake. Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake. Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake. Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama BWANA alivyomwamuru Mose.’ ”