Hesabu 27
27
Haki ya kurithi kwa wanawake
1Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirza walikuwa binti zake Selofehadi. Naye Selofehadi alikuwa mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase mwanawe Yosefu. 2Basi, hao binti wanne walimwendea Mose, wakasimama mbele yake na kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya ya Waisraeli, kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasema, 3“Baba yetu alifia jangwani nyikani na bila mtoto yeyote wa kiume. 4Yeye hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora waliokusanyika dhidi ya Mwenyezi-Mungu, bali alikufa kutokana na dhambi yake mwenyewe. Kwa nini basi jina la baba yetu lifutwe katika ukoo wake kwa sababu hakuwa na mtoto wa kiume? Tupe urithi pamoja na ndugu zake baba yetu.”
5Mose akaleta lalamiko lao mbele ya Mwenyezi-Mungu. 6Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 7#Taz Hes 36:2 “Wanachosema binti za Selofehadi ni kweli; wape urithi pamoja na ndugu za baba yao, wachukue urithi wake. 8Kisha waambie Waisraeli kwamba mtu yeyote akifa bila kuacha mtoto wa kiume, urithi wake atapewa binti yake. 9Ikiwa hana binti, basi urithi huo watapewa ndugu zake wa kiume. 10Na ikiwa hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utawaendea baba zake, wakubwa na wadogo. 11Na ikiwa baba yake hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utakuwa wa jamaa yake wa karibu, naye ataumiliki kama mali yake. Hii itakuwa kanuni na sheria kwa Waisraeli, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyokuamuru.”
Yoshua ateuliwa kuwaongoza Waisraeli
(Kumb 31:1-8)
12 # Taz Kumb 3:23-27; 32:48-52; Marko 6:34 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Panda juu ya Mlima huu wa miinuko ya Abarimu uitazame nchi ambayo nimewapa Waisraeli. 13Ukisha iona, nawe pia utafariki kama ndugu yako Aroni alivyofariki, 14kwa sababu hamkuitii amri yangu kule jangwani Sini. Wakati jumuiya yote ya watu walipolalamika juu yangu kule Meriba, hamkuacha utukufu wangu uonekane mbele yao walipotaka wapewe maji.” (Meriba ni chemchemi ya maji ya Kadeshi katika jangwa la Sini).
15Naye Mose akamwomba Mwenyezi-Mungu, 16“Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu uliye asili ya uhai wote,#27:16 Mungu uliye asili ya uhai wote: Neno kwa neno: Mungu wa roho za wanaadamu wote. nakuomba umteue mtu wa kuisimamia jumuiya hii, 17#Taz 1Fal 22:17; Eze 34:5; Mat 9:36 ambaye atawatangulia na kuwaongoza katika shughuli zao zote, ili wasije wakawa kama kondoo wasio na mchungaji.”
18 # Taz Kut 24:13 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtwae Yoshua mwana wa Nuni, mtu mwenye roho nzuri, kisha umwekee mikono, 19na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote, umkabidhi jukumu hilo. 20Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli imtii. 21#Taz Kut 28:30; 1Sam 14:41; 28:6 Yeye atamtegemea kuhani Eleazari ambaye atamjulisha matakwa yangu kwa kutumia jiwe la kauli.#27:21 jiwe la kauli: Kiebrania: Urimu, moja ya mawe mawili yaliyotumiwa na kuhani kujua matakwa ya Mungu. Kwa njia hii, Eleazari atamwongoza Yoshua na jumuiya yote ya Waisraeli wanapotoka na wanapoingia.” 22Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alimtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote ya Waisraeli. 23#Taz Kumb 31:23 Kisha akamwekea mikono kichwani na kumpa mamlaka kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
Hesabu 27: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.