Isaya 33:1-9
Isaya 33:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wako ewe mwangamizi, unayeangamiza bila wewe kuangamizwa! Ole wako wewe mtenda hila, ambaye hakuna aliyekutendea hila! Utakapokwisha kuangamiza wewe utaangamizwa! Utakapomaliza kuwatendea watu hila wewe utatendewa hila. Ee Mwenyezi-Mungu, utuonee huruma, kwako tumeliweka tumaini letu. Uwe kinga yetu kila siku, wokovu wetu wakati wa taabu. Kwa kishindo cha sauti yako watu hukimbia; unapoinuka tu, mataifa hutawanyika. Maadui zao wanakusanya mateka, wanayarukia kama panzi. Mwenyezi-Mungu ametukuka, yeye anaishi juu mbinguni. Ameujaza Siyoni haki na uadilifu. Enyi watu wa Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu atawajalieni usalama, atawaokoa na kuwapa hekima na maarifa. Hazina yenu kuu ni kumcha Mwenyezi-Mungu. Haya, mashujaa wao wanalia, wajumbe wa amani wanaomboleza. Barabara kuu zimebaki tupu; hamna anayesafiri kupitia humo. Mikataba inavunjwa ovyo, mashahidi wanadharauliwa. Hamna anayejali tena maisha ya binadamu. Nchi inaomboleza na kunyauka; misitu ya Lebanoni imekauka, bonde zuri la Sharoni limekuwa jangwa, huko Bashani na mlimani Karmeli miti imepukutika majani yake.
Isaya 33:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe. Ee BWANA, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asububi, na wokovu wetu pia wakati wa taabu. Makabila ya watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako. Na mateka yako yatakukusanywa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige. BWANA ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki. Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha BWANA ni hazina yake ya akiba. Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu. Njia kuu zimeachwa, msafiri ameikimbia barabara; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu. Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.
Isaya 33:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe. Ee BWANA, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asububi, na wokovu wetu pia wakati wa taabu. Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako. Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige. BWANA ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki. Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha BWANA ni hazina yake ya akiba. Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu. Njia kuu zimeachwa, msafiri amekoma; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu. Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.
Isaya 33:1-9 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ole wako wewe, ee mharibu, wewe ambaye hukuharibiwa! Ole wako, ee msaliti, wewe ambaye hukusalitiwa! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa; utakapokwisha kusaliti, utasalitiwa. Ee Mwenyezi Mungu, uturehemu, tunakutamani. Uwe nguvu yetu kila asubuhi na wokovu wetu wakati wa taabu. Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia; unapoinuka, mataifa hutawanyika. Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa kama wafanyavyo madumadu, watu huvamia juu yake kama kundi la nzige. Mwenyezi Mungu ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka, ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu. Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu, hazina ya wokovu tele, hekima na maarifa; kumcha Mwenyezi Mungu ni ufunguo wa hazina hii. Angalia, mashujaa wake wanapiga kelele barabarani, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu. Njia kuu zimeachwa, hakuna wasafiri barabarani. Mkataba umevunjika, mashahidi wake wamedharauliwa, hakuna anayeheshimiwa. Ardhi inaomboleza na kuchakaa, Lebanoni imeaibika na kunyauka; Sharoni ni kama Araba, nayo Bashani na Karmeli wanapukutisha majani yao.