Isaya 33
33
Taabu na msaada
1Ole wako wewe, ee mharibu,
wewe ambaye hukuharibiwa!
Ole wako, ee msaliti,
wewe ambaye hukusalitiwa!
Utakapokwisha kuharibu,
utaharibiwa;
utakapokwisha kusaliti,
utasalitiwa.
2Ee Mwenyezi Mungu, uturehemu,
tunakutamani.
Uwe nguvu yetu kila asubuhi
na wokovu wetu wakati wa taabu.
3Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia;
unapoinuka, mataifa hutawanyika.
4Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa
kama wafanyavyo madumadu,
watu huvamia juu yake
kama kundi la nzige.
5Mwenyezi Mungu ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka,
ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu.
6Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu,
hazina ya wokovu tele, hekima na maarifa;
kumcha Mwenyezi Mungu ni ufunguo wa hazina hii.
7Angalia, mashujaa wake wanapiga kelele barabarani,
wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.
8Njia kuu zimeachwa,
hakuna wasafiri barabarani.
Mkataba umevunjika,
mashahidi wake wamedharauliwa#33:8 au miji yake imedharauliwa,
hakuna anayeheshimiwa.
9Ardhi inaomboleza#33:9 au Ardhi inakauka na kuchakaa,
Lebanoni imeaibika na kunyauka;
Sharoni ni kama Araba,
nayo Bashani na Karmeli
wanapukutisha majani yao.
10“Sasa nitainuka,” asema Mwenyezi Mungu.
“Sasa nitatukuzwa;
sasa nitainuliwa juu.
11Mlichukua mimba ya makapi,
mkazaa mabua;
pumzi yenu ni moto unaowateketeza.
12Mataifa watachomwa wawe majivu;
kama vichaka vya miiba vilivyokatwa ndivyo watakavyochomwa.”
13Ninyi mlio mbali sana, sikieni lile nililofanya;
ninyi mlio karibu, tambueni uweza wangu!
14Wenye dhambi katika Sayuni wametiwa hofu,
kutetemeka kumewakumba wasiomcha Mungu:
“Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto ulao?
Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto unaowaka milele?”
15Yeye aendaye kwa uadilifu
na kusema lililo haki,
yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma
na kuizuia mikono yake isipokee rushwa,
yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji,
na yeye afumbaye macho yake yasitazame uovu:
16huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu,
ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani.
Atapewa mkate wake,
na maji yake hayatakoma.
17Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake
na kuiona nchi inayoenea mbali.
18Katika mawazo yenu mtaifikiria hofu iliyopita:
“Yuko wapi yule afisa mkuu?
Yuko wapi yule aliyechukua ushuru?
Yuko wapi afisa msimamizi wa minara?”
19Hutawaona tena wale watu wenye kiburi,
wale watu wenye usemi wa mafumbo,
wenye lugha ngeni, isiyoeleweka.
20Mtazame Sayuni, mji wa sikukuu zetu;
macho yenu yatauona Yerusalemu,
mahali pa amani pa kuishi, hema ambalo halitaondolewa,
nguzo zake hazitang’olewa kamwe,
wala hakuna kamba yake yoyote itakayokatika.
21Huko Mwenyezi Mungu atakuwa Mwenye Nguvu wetu.
Patakuwa kama mahali pa mito mipana na vijito.
Hakuna jahazi lenye makasia litakalopita huko,
wala hakuna meli yenye nguvu itakayopita huko.
22Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwamuzi wetu,
Mwenyezi Mungu ndiye mtoa sheria wetu,
Mwenyezi Mungu ni mfalme wetu,
yeye ndiye atakayetuokoa.
23Kamba zenu za merikebu zimelegea:
Mlingoti haukusimama imara,
nalo tanga halikukunjuliwa.
Wingi wa mateka yatagawanywa,
hata yeye aliye mlemavu atachukua nyara.
24Hakuna yeyote aishiye Sayuni atakayesema,
“Mimi ni mgonjwa”;
nazo dhambi za wale wanaoishi humo
zitasamehewa.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 33: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.