Isaya 32
32
Ufalme wa haki
1Tazama, mfalme atatawala kwa uadilifu
na watawala watatawala kwa haki.
2Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo
na kimbilio kutokana na dhoruba,
kama vijito vya maji jangwani
na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu.
3Ndipo macho ya wale wanaoona hayatafumbwa tena,
nayo masikio ya wale wanaosikia yatasikiliza.
4Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa,
nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha.
5Mpumbavu hataitwa tena muungwana,
wala mtu mbaya kabisa kupewa heshima ya juu.
6Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu,
moyo wake hushughulika na uovu:
Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu,
na hueneza habari za makosa kuhusu Mwenyezi Mungu;
yeye huwaacha wenye njaa bila kitu,
na wenye kiu huwanyima maji.
7Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu,
hufanya mipango miovu
ili kumwangamiza maskini kwa uongo,
hata wakati hoja za mhitaji ni za haki.
8Lakini mtu muungwana hufanya mipango ya kiungwana,
na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa.
Wanawake wa Yerusalemu
9Enyi wanawake wenye kuridhika sana,
amkeni na mnisikilize.
Enyi binti mnaojisikia kuwa salama,
sikieni lile ninalotaka kuwaambia!
10Muda zaidi kidogo ya mwaka mmoja,
ninyi mnaojisikia salama mtatetemeka,
mavuno ya zabibu yatakoma,
na mavuno ya matunda hayatakuwepo.
11Tetemekeni, enyi wanawake wenye kuridhika,
tetemekeni kwa hofu, enyi binti mnaojisikia salama!
Vueni nguo zenu,
vaeni magunia viunoni mwenu.
12Pigeni vifua vyenu, mlilie mashamba yenu mazuri,
kwa ajili ya mizabibu iliyozaa vizuri
13na kwa ajili ya nchi ya watu wangu,
nchi ambayo miiba na michongoma imemea:
naam, ombolezeni kwa ajili ya nyumba zote za furaha
na kwa ajili ya mji huu wenye kufanya sherehe.
14Ngome itaachwa,
mji wenye kelele nyingi utahamwa,
ngome ndani ya mji na mnara wa ulinzi vitakuwa ukiwa milele,
mahali pazuri pa punda-mwitu na malisho ya makundi ya kondoo,
15hadi Roho wa Mungu amwagwe juu yetu kutoka juu,
nalo jangwa kuwa shamba lenye rutuba,
na shamba lenye rutuba kuwa kama msitu.
16Haki itakaa katika jangwa,
na uadilifu utakaa katika shamba lenye rutuba.
17Matunda ya haki yatakuwa amani,
matokeo ya haki yatakuwa utulivu
na matumaini milele.
18Watu wangu wataishi katika makao ya mahali pa amani,
katika nyumba zilizo salama,
katika mahali pa kupumzika pasipo na usumbufu.
19Hata mvua ya mawe iangushe msitu
na mji ubomolewe kabisa,
20tazama jinsi utakavyobarikiwa,
ukipanda mbegu yako katika kila kijito,
na kuwaacha ng’ombe wako
na punda wajilishe kwa uhuru.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 32: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.