Isaya 34
34
Hukumu dhidi ya mataifa
1Njooni karibu, enyi mataifa, nanyi msikilize;
sikilizeni kwa makini,
enyi makabila ya watu!
Dunia na isikie, navyo vyote vilivyo ndani yake,
ulimwengu na vyote vinavyotoka ndani yake!
2Mwenyezi Mungu ameyakasirikia mataifa yote;
ghadhabu yake ni juu ya majeshi yao yote.
Atawaangamiza kabisa,
atawatia mikononi mwa wachinjaji.
3Waliouawa watatupwa nje,
maiti zao zitatoa uvundo,
milima itatota kwa damu zao.
4Nyota zote za mbinguni zitayeyuka
na mbingu itakunjwa kama kitabu,
jeshi lote la angani litaanguka
kama majani yaliyonyauka kwenye mzabibu,
kama tini iliyonyauka kwenye mtini.
5Upanga wangu umekunywa na kushiba huko mbinguni,
tazama, unashuka katika hukumu juu ya Edomu,
wale watu ambao nimeshawahukumu,
kuwaangamiza kabisa.
6Upanga wa Mwenyezi Mungu umeoga katika damu,
umefunikwa na mafuta ya nyama:
damu ya kondoo na mbuzi,
mafuta kutoka figo za kondoo dume.
Kwa maana Mwenyezi Mungu ana dhabihu huko Bosra,
na machinjo makuu huko Edomu.
7Nyati wataanguka pamoja nao,
ndama dume na mafahali wakubwa.
Nchi yao italowana kwa damu,
nayo mavumbi yataloa mafuta ya nyama.
8Kwa sababu Mwenyezi Mungu anayo siku ya kulipiza kisasi,
mwaka wa malipo,
siku ya kushindania shauri la Sayuni.
9Vijito vya Edomu vitageuka kuwa lami,
mavumbi yake yatakuwa kiberiti kiunguzacho,
nchi yake itakuwa lami iwakayo!
10Haitazimishwa usiku wala mchana,
moshi wake utapaa juu milele.
Kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa;
hakuna mtu yeyote atakayepita huko tena.
11Bundi wa jangwani na bundi mwenye sauti nyembamba wataimiliki,
bundi wakubwa na kunguru wataweka viota humo.
Mungu atanyoosha juu ya Edomu
kamba ya kupimia ya machafuko matupu,
na timazi ya ukiwa.
12Watu wake wa kuheshimiwa hawatakuwa na chochote
kitakachoitwa ufalme huko,
nao wakuu wao wote watatoweka.
13Miiba itaenea katika ngome za ndani,
viwawi na michongoma itaota
kwenye ngome zake.
Itakuwa maskani ya mbweha,
makao ya bundi.
14Viumbe vya jangwani vitakutana na fisi,
nao mbuzi-mwitu watalia wakiitana;
huko viumbe vya usiku vitastarehe pia
na kujitafutia mahali pa kupumzika.
15Bundi wataweka viota huko na kutaga mayai,
atayaangua na kutunza makinda yake
chini ya uvuli wa mabawa yake;
pia huko vipanga watakusanyika,
kila mmoja na mwenzi wake.
16Angalieni katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na msome:
Hakuna hata mmoja katika hawa atakayekosekana,
hakuna hata mmoja atakayemkosa mwenzi wake.
Kwa kuwa ni kinywa chake Mungu kimeagiza,
na Roho wake Mtakatifu atawakusanya.
17Huwagawia sehemu zao,
mkono wake huwagawanyia kwa kipimo.
Wataimiliki hata milele
na kuishi humo kizazi hadi kizazi.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 34: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.