Isaya 33:1-9
Isaya 33:1-9 BHN
Ole wako ewe mwangamizi, unayeangamiza bila wewe kuangamizwa! Ole wako wewe mtenda hila, ambaye hakuna aliyekutendea hila! Utakapokwisha kuangamiza wewe utaangamizwa! Utakapomaliza kuwatendea watu hila wewe utatendewa hila. Ee Mwenyezi-Mungu, utuonee huruma, kwako tumeliweka tumaini letu. Uwe kinga yetu kila siku, wokovu wetu wakati wa taabu. Kwa kishindo cha sauti yako watu hukimbia; unapoinuka tu, mataifa hutawanyika. Maadui zao wanakusanya mateka, wanayarukia kama panzi. Mwenyezi-Mungu ametukuka, yeye anaishi juu mbinguni. Ameujaza Siyoni haki na uadilifu. Enyi watu wa Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu atawajalieni usalama, atawaokoa na kuwapa hekima na maarifa. Hazina yenu kuu ni kumcha Mwenyezi-Mungu. Haya, mashujaa wao wanalia, wajumbe wa amani wanaomboleza. Barabara kuu zimebaki tupu; hamna anayesafiri kupitia humo. Mikataba inavunjwa ovyo, mashahidi wanadharauliwa. Hamna anayejali tena maisha ya binadamu. Nchi inaomboleza na kunyauka; misitu ya Lebanoni imekauka, bonde zuri la Sharoni limekuwa jangwa, huko Bashani na mlimani Karmeli miti imepukutika majani yake.