Wagalatia 6:1-10
Wagalatia 6:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote. Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
Wagalatia 6:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, nyinyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa. Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo. Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe. Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine. Maana kila mmoja anapaswa kuubeba mzigo wake mwenyewe. Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake. Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uhai wa milele. Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.
Wagalatia 6:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, mtu akishikwa katika kosa lolote, ninyi mlio wa Roho mrejesheni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na hivyo kuitimiza sheria ya Kristo. Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake. Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. Mwanafunzi na amshirikishe mwalimu wake katika mema yote. Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.
Wagalatia 6:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo. Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake. Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe. Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote. Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.