Wagalatia 6:1-10
Wagalatia 6:1-10 BHN
Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, nyinyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa. Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo. Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe. Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine. Maana kila mmoja anapaswa kuubeba mzigo wake mwenyewe. Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake. Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uhai wa milele. Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.