Wagalatia 6
6
Tuvumiliane na kusaidiana
1Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, nyinyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa. 2Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo. 3Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe. 4Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine. 5Maana kila mmoja anapaswa kuubeba mzigo wake mwenyewe.
6Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.
7Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. 8Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uhai wa milele. 9Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. 10Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.
Mawaidha ya mwisho na salamu
11Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe. 12Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha nyinyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: Kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. 13Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; huwataka nyinyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu. 14Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. 15Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya. 16Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli – watu wa Mungu.
17Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu.
18Ndugu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amina.
Iliyochaguliwa sasa
Wagalatia 6: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.