Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 2:18-29

Ufunuo 2:18-29 BHN

“Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi: “Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang'aa kama shaba iliyosuguliwa. Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali. Lakini nina jambo moja dhidi yako: Wewe unamvumilia yule mwanamke Yezebeli anayejiita nabii, anayefundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu. Nimempa muda wa kutubu, lakini hataki kuachana na uzinzi wake. Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye. Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu. “Lakini nyinyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezebeli na ambao hamkujifunza kile wanachokiita Siri ya Shetani, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine. Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja. “Mshindi na mwenye kuzingatia mpaka mwisho mambo ninayotaka, nitampa mamlaka juu ya watu wa mataifa: Atawaongoza kwa fimbo ya chuma na kuwavunjavunja kama vyombo vya udongo. Mimi pia nimepokea mamlaka hayo kutoka kwa Baba yangu. Tena nitampa nyota ya asubuhi. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!