Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 2:18-29

Ufunuo 2:18-29 NEN

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika: “Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza. “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki. Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo yanayoitwa mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wowote juu yenu): Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja. “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa: “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma, atawavunja vipande vipande kama chombo cha udongo’: kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu. Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi. Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.