Ufunuo 2:18-29
Ufunuo 2:18-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika: “Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza. “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki. Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo yanayoitwa mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wowote juu yenu): Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja. “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa: “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma, atawavunja vipande vipande kama chombo cha udongo’: kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu. Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi. Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.
Ufunuo 2:18-29 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi: “Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang'aa kama shaba iliyosuguliwa. Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali. Lakini nina jambo moja dhidi yako: Wewe unamvumilia yule mwanamke Yezebeli anayejiita nabii, anayefundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu. Nimempa muda wa kutubu, lakini hataki kuachana na uzinzi wake. Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye. Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu. “Lakini nyinyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezebeli na ambao hamkujifunza kile wanachokiita Siri ya Shetani, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine. Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja. “Mshindi na mwenye kuzingatia mpaka mwisho mambo ninayotaka, nitampa mamlaka juu ya watu wa mataifa: Atawaongoza kwa fimbo ya chuma na kuwavunjavunja kama vyombo vya udongo. Mimi pia nimepokea mamlaka hayo kutoka kwa Baba yangu. Tena nitampa nyota ya asubuhi. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!
Ufunuo 2:18-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama muali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye fikira na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wowote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine. Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja. Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu. Nami nitampa ile nyota ya asubuhi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho anayaambia makanisa.
Ufunuo 2:18-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine. Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja. Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu. Nami nitampa ile nyota ya asubuhi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.