Zaburi 84:5-12
Zaburi 84:5-12 BHN
Heri watu wanaopata nguvu zao kwako, wanaotamani kwenda kuhiji mlimani kwako. Wapitapo katika bonde kavu la Baka, hulifanya kuwa mahali pa chemchemi, na mvua za vuli hulijaza madimbwi. Wanaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi; watamwona Mungu wa miungu huko Siyoni. Usikie sala yangu ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi; unitegee sikio, ee Mungu wa Yakobo. Ee Mungu, umwangalie kwa wema ngao yetu mfalme, umtazame huyo uliyemweka wakfu kwa mafuta. Siku moja tu katika maskani yako, ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali kusimama mlangoni pa nyumba yako, kuliko kuishi nyumbani kwa watu waovu. Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu; yeye hutuneemesha na kutujalia fahari. Hawanyimi chochote kilicho chema, wale waishio kwa unyofu. Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, heri mtu yule anayekutumainia wewe!