Zaburi 68:19-27
Zaburi 68:19-27 BHN
Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku! Yeye hutubebea mizigo yetu; yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu. Mungu wetu ni Mungu mwenye kutuokoa; Bwana Mungu pekee ndiye aokoaye katika kifo. Mungu ataviponda vichwa vya maadui zake, naam, vichwa vya wanaoshikilia njia mbaya. Bwana alisema: “Nitawarudisha maadui kutoka Bashani; nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari, uoshe miguu katika damu ya maadui zako, nao mbwa wako wale shibe yao.” Ee Mungu, misafara yako ya ushindi yaonekana; misafara ya Mungu wangu, mfalme wangu, hadi patakatifu pake! Mbele waimbaji, nyuma wanamuziki, katikati wasichana wanavumisha vigoma. “Msifuni Mungu katika jumuiya kubwa ya watu. Msifuni Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Israeli!” Kwanza ni Benyamini, mdogo wa wote; kisha viongozi wa Yuda na kundi lao, halafu wakuu wa Zebuluni na Naftali.