Zaburi 36:1-12
Zaburi 36:1-12 BHN
Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake; jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Mwovu hujipendelea mwenyewe, hufikiri uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, hujiweka katika njia isiyo njema, wala haachani na uovu. Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni; uaminifu wako wafika mawinguni. Uadilifu wako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama vilindi vya bahari. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako! Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako. Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako; wawanywesha kutoka mto wa wema wako. Wewe ndiwe asili ya uhai; kwa mwanga wako twaona mwanga. Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua; uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo. Usikubali wenye majivuno wanivamie, wala watu waovu wanikimbize. Kumbe watendao maovu wameanguka; wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.