Zaburi 36:1-12
Zaburi 36:1-12 NENO
Kuna neno moyoni mwangu kutoka kwa Mungu kuhusu hali ya dhambi ya mwovu. Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake. Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake. Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu, ameacha kuwa mwenye hekima au kutenda mema. Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya, hujitia katika njia ya dhambi na hakatai lililo baya. Upendo wako, Ee BWANA, unafika hadi mbinguni, uaminifu wako hadi kwenye anga. Haki yako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama kilindi kikuu. Ee BWANA, wewe huwahifadhi mwanadamu na mnyama. Upendo wako usiokoma ni wa thamani mno! Watu wakuu na wadogo hujificha uvulini wa mabawa yako. Wanajifurahisha katika wingi ulio nyumbani mwako, nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako. Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima, katika nuru yako twaona nuru. Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe, haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo. Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu, wala mkono wa mwovu usinifukuze. Tazama jinsi watenda maovu walivyoanguka: wametupwa chini, hawawezi kuinuka!