Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 31:1-16

Zaburi 31:1-16 BHN

Kwako, ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama, usiniache niaibike kamwe; kwa uadilifu wako uniokoe. Unitegee sikio, uniokoe haraka! Uwe kwangu mwamba wa usalama, ngome imara ya kuniokoa. Naam, wewe ni mwamba wangu na ngome yangu; kwa hisani yako uniongoze na kunielekeza. Unitoe katika mtego walionitegea mafichoni; maana wewe ni kimbilio la usalama wangu. Mikononi mwako naiweka roho yangu; umenikomboa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwaminifu. Wawachukia wanaoabudu sanamu batili; lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu. Nitashangilia na kufurahia fadhili zako, maana wewe waiona dhiki yangu, wajua na taabu ya nafsi yangu. Wewe hukuniacha nitiwe mikononi mwa maadui zangu; umenisimamisha mahali pa usalama. Unionee huruma, ee Mwenyezi-Mungu, niko taabuni; macho yangu yamechoka kwa huzuni, nimeishiwa nguvu mwilini na rohoni. Maisha yangu yamekwisha kwa majonzi; naam, miaka yangu kwa kulalamika. Nguvu zangu zimeniishia kwa kutaabika; hata mifupa yangu imekauka. Nimekuwa dharau kwa maadui zangu wote; kioja kwa majirani zangu. Rafiki zangu waniona kuwa kitisho; wanionapo njiani hunikimbia. Nimesahaulika kama mtu aliyekufa; nimekuwa kama chungu kilichovunjikavunjika. Nasikia watu wakinongonezana, vitisho kila upande; wanakula njama dhidi yangu, wanafanya mipango ya kuniua. Lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu. Nasema: “Wewe ni Mungu wangu!” Maisha yangu yamo mikononi mwako; uniokoe na maadui zangu, niokoe na hao wanaonidhulumu. Uniangalie kwa wema mimi mtumishi wako; uniokoe kwa fadhili zako.

Soma Zaburi 31