Zaburi 18:16-30
Zaburi 18:16-30 BHN
Mungu alinyosha mkono kutoka juu akanichukua, kutoka katika maji mengi alininyanyua. Aliniokoa kutoka kwa maadui zangu wenye nguvu nyingi, aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia, maana walikuwa na nguvu kunishinda. Walinivamia nilipokuwa taabuni, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu. Alinileta, akaniweka mahali pa usalama; alinisalimisha, kwani alipendezwa nami. Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu; alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia. Maana nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu, wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu. Nimeshika maagizo yake yote, sikuacha kufuata masharti yake. Mbele yake sikuwa na hatia; nimejikinga nisiwe na hatia. Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu; yeye ajua kwamba mikono yangu haina hatia. Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu; mwema kwa wale walio wema. Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu; lakini mkatili kwa watu walio waovu. Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu, lakini wenye majivuno huwaporomosha. Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia; walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Kwa msaada wako nakishambulia kikosi; wewe wanipa nguvu ya kuruka ukuta. Huyu Mungu matendo yake hayana dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia usalama.