Zaburi 18:16-30
Zaburi 18:16-30 NEN
Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu. Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini BWANA alikuwa msaada wangu. Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa. Kwa maana nimezishika njia za BWANA; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu. Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake. Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi. BWANA amenilipa sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake. Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionyesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia, unajionyesha kutokuwa na hatia. Kwa aliye mtakatifu, unajionyesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka, unajionyesha kuwa mkaidi. Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini huwashusha wenye kiburi. Wewe, Ee BWANA, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka; Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga. Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta. Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu, neno la BWANA halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake.