Zaburi 145:11-21
Zaburi 145:11-21 BHN
Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako, na kutangaza juu ya nguvu yako kuu, ili kila mtu ajue matendo yako makuu, na fahari tukufu ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele; mamlaka yako yadumu vizazi vyote. Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote, ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka; huwainua wote waliokandamizwa. Viumbe vyote vinakutazama kwa hamu, nawe wavipa chakula chao kwa wakati wake. Waufumbua mkono wako kwa ukarimu, watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai. Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu katika njia zake zote; ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba, wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu. Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha; husikia kilio chao na kuwaokoa. Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wanaompenda; lakini atawaangamiza waovu wote. Nitatangaza sifa za Mwenyezi-Mungu; viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu, milele na milele.