Methali 12:11-23
Methali 12:11-23 BHN
Mkulima mwenye bidii ana chakula tele, lakini afuataye mambo yasiyofaa hana akili. Waovu hutamani faida isiyo halali, lakini mtu mwadilifu husimama imara. Mtu mwovu hunaswa kwa uongo wake mwenyewe, lakini mwadilifu hutoka katika taabu. Mtu hufanikiwa kutokana na maneno yake kama apatavyo matokeo ya kazi za mikono yake. Mpumbavu huiona njia yake kuwa sawa, lakini mwenye hekima husikiliza shauri. Udhia wa mpumbavu hujulikana mara, lakini mwerevu huyapuuza matukano. Msema kweli hutoa ushahidi wa kweli, lakini shahidi wa uongo hutamka udanganyifu. Maneno ya ovyo hujeruhi kama upanga, lakini asemayo mwenye hekima huponesha kidonda. Ukweli hudumu milele, lakini uongo ni wa kitambo tu. Wanaopanga maovu wamejaa udanganyifu moyoni, lakini wanaonuia mema hupata furaha. Waadilifu hawapatwi na jambo lolote baya, lakini waovu wamejaa dhiki. Midomo isemayo uongo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini watu waaminifu ni furaha yake. Mwenye busara huficha maarifa yake, lakini wapumbavu hutangaza upumbavu wao.