Mathayo 6:7-15
Mathayo 6:7-15 BHN
“Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi. Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba. Basi, hivi ndivyo mnavyopaswa kusali: ‘Baba yetu uliye mbinguni: Jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo chakula chetu cha kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea. Usitutie katika majaribu, lakini utuokoe na yule Mwovu.’ [ Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] “Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu.