Yeremia 10:1-16
Yeremia 10:1-16 BHN
Sikilizeni neno analowaambieni Mwenyezi-Mungu, enyi Waisraeli! Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Msijifunze mienendo ya mataifa mengine, wala msishangazwe na ishara za mbinguni; yaacheni mataifa mengine yashangazwe nazo. Maana, mila za dini za watu hawa ni za uongo. Mtu hukata mti msituni fundi akachonga kinyago cha mungu kwa shoka. Kisha watu hukipamba kwa fedha na dhahabu wakakipigilia misumari kwa nyundo ili kisije kikaanguka. Vinyago vyao ni kama vinyago vya kutishia ndege katika shamba la matango, havina uwezo wa kuongea; ni lazima vibebwe maana haviwezi kutembea. Msiviogope vinyago hivyo, maana haviwezi kudhuru, wala haviwezi kutenda lolote jema.” Ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe; wewe ni mkuu na nguvu yako yajulikana. Nani asiyekuogopa wewe, ee mfalme wa mataifa? Wewe wastahili kuheshimiwa. Miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika falme zao zote, hakuna hata mmoja aliye kama wewe. Wote ni wajinga na wapumbavu mafunzo ya vinyago ni upuuzi mtupu! Vinyago hivyo hupambwa kwa fedha kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ofiri; kazi ya mafundi stadi na wafua dhahabu. Zimevishwa nguo za samawati na zambarau, zilizofumwa na wafumaji stadi. Lakini Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa kweli; Mungu aliye hai, mfalme wa milele. Akikasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake. Basi, utawaambia hivi: “Miungu ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia. Itatoweka kabisa duniani na chini ya mbingu.” Mwenyezi-Mungu aliiumba dunia kwa nguvu zake; kwa hekima yake aliuimarisha ulimwengu, kwa akili yake alizitandaza mbingu. Anapotoa sauti yake, maji hunguruma mbinguni, huzusha ukungu kutoka mipaka ya dunia. Huufanya umeme umulike wakati wa mvua, na kuutoa upepo katika ghala zake. Binadamu ni mjinga na mpumbavu; kila mfua dhahabu huaibishwa na vinyago vyake; maana, vinyago hivyo ni uongo mtupu. Havina uhai wowote ndani yao. Havina thamani, ni udanganyifu mtupu; wakati vitakapoadhibiwa vyote vitaangamia. Lakini Mungu wa Yakobo si kama vinyago hivyo, maana, yeye ndiye aliyeumba vitu vyote, na Israeli ni taifa lililo mali yake; Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndilo jina lake.