Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 10:1-16

Yeremia 10:1-16 NEN

Sikieni lile ambalo BWANA, anena nanyi ee nyumba ya Israeli. Hili ndilo asemalo BWANA: “Usijifunze njia za mataifa wala usitishwe na ishara katika anga, ingawa mataifa yanatishwa nazo. Kwa maana desturi za mataifa hazina maana, wanakata mti msituni, na fundi anauchonga kwa patasi. Wanaparemba kwa fedha na dhahabu, wanakikaza kwa nyundo na misumari ili kisitikisike. Sanamu zao ni kama sanamu iliyowekwa shambani la matango kutishia ndege nazo haziwezi kuongea; sharti zibebwe sababu haziwezi kutembea. Usiziogope; haziwezi kudhuru, wala kutenda lolote jema.” Hakuna aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ni mkuu, jina lako ni lenye nguvu katika uweza. Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe, Ee Mfalme wa mataifa? Hii ni stahili yako. Miongoni mwa watu wote wenye hekima katika mataifa na katika falme zao zote, hakuna aliye kama wewe. Wote hawana akili, tena ni wapumbavu, wanafundishwa na sanamu za miti zisizofaa lolote. Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi na dhahabu kutoka Ufazi. Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani: vyote vikiwa vimetengenezwa na mafundi stadi. Lakini BWANA ni Mungu wa kweli, yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele. Anapokasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake. “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ” Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake, akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake, na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake. Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma; huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia. Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua, naye huuleta upepo kutoka ghala zake. Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa, kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. Vinyago vyake ni vya udanganyifu, havina pumzi ndani yavyo. Havifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha tu, hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia. Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo, kwani ndiye Muumba wa vitu vyote, pamoja na Israeli, kabila la urithi wake: BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.