Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yer 10:1-16

Yer 10:1-16 SUV

Enyi nyumba ya Israeli, lisikieni neno awaambialo BWANA; BWANA asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo. Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka. Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike. Mfano wao ni mfano wa mtende, kazi ya cherehani, hawasemi; hawana budi kuchukuliwa, kwa sababu hawawezi kwenda. Usiwaogope; kwa maana hawawezi kutenda uovu, wala hawana uwezo wa kutenda mema. Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza. Ni nani asiyekucha wewe, Ee mfalme wa mataifa? Maana hii ni sifa yako wewe; kwa kuwa miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika hali yao ya enzi yote pia, hapana hata mmoja kama wewe. Lakini wote pia huwa kama wanyama, ni wapumbavu. Haya ni maelezo ya sanamu, ni shina la mti tu. Iko fedha iliyofuliwa ikawa mabamba, iliyoletwa kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ufazi, kazi ya stadi na ya mikono ya mfua dhahabu; mavazi yao ni rangi ya samawi na urujuani; hayo yote ni kazi ya mafundi yao. Bali BWANA ndiye Mungu wa kweli; Ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele; Mbele za ghadhabu yake nchi yatetemeka, Wala mataifa hawawezi kustahimili hasira yake. Mtawaambia hivi, Miungu hiyo isiyofanya mbingu na nchi, hiyo itaangamia katika nchi, nayo itatoweka chini ya mbingu. Ameiumba dunia kwa uweza wake, Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu. Atoapo sauti yake, pana mshindo wa maji mbinguni, Naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi; Huifanyia mvua umeme, Huutoa upepo katika hazina zake. Kila mtu amekuwa kama mnyama, hana maarifa; Kila mfua dhahabu amefedheheshwa na sanamu yake ya kuchonga; Maana sanamu yake ya kuyeyuka ni uongo, Wala hamna pumzi ndani yake. Ni ubatili tu, ni kazi za udanganyifu; Wakati wa kujiliwa kwao watapotea. Yeye, Fungu la Yakobo, siye kama hawa; Maana ndiye aliyeviumba vitu vyote; Na Israeli ni kabila ya urithi wake; BWANA wa majeshi ndilo jina lake.

Soma Yer 10