Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 14:24-32

Isaya 14:24-32 BHN

Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameapa: “Kama nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa; kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyokamilika. Nitauvunja uwezo wa Waashuru nchini mwangu; nitawakanyagakanyaga katika milima yangu. Nitawaondolea watu wangu nira ya dhuluma yao, na mzigo wa mateso yao.” Huu ndio uamuzi wake Mwenyezi-Mungu kuhusu dunia yote; hii ndiyo adhabu atakayotoa juu ya mataifa yote. Kama Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameamua, nani atakayeweza kubatilisha uamuzi wake? Kama amepania kutoa adhabu, ni nani atakayempinga? Mwaka alipofariki mfalme Ahazi, Mungu alitoa kauli hii: “Msishangilie enyi Wafilisti wote, kwamba Ashuru, fimbo iliyowapiga, imevunjika; maana, nyoka wa kawaida atazaa nyoka mwenye sumu, na nyoka mwenye sumu atazaa joka lirukalo. Wazaliwa wa kwanza wa maskini watashiba, na fukara watakaa kwa usalama. Lakini chipukizi wenu nitawaua kwa njaa; na yeyote wenu atakayebaki nitamuua. Piga yowe ewe lango; lia ewe mji; yeyuka kwa hofu ewe nchi yote ya Filistia. Maana moshi wa askari waja kutoka kaskazini, wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.” Basi watapewa jibu gani wajumbe wa taifa hilo? Wataambiwa: Mwenyezi-Mungu ameijenga imara Siyoni, na maskini wa watu wake watakimbilia usalama huko.

Soma Isaya 14