Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 16:7-16

Mwanzo 16:7-16 BHN

Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamkuta Hagari penye chemchemi ya maji jangwani, chemchemi iliyoko njiani kuelekea Shuri. Malaika akamwuliza, “Hagari, mjakazi wa Sarai! Unatoka wapi na unakwenda wapi?” Hagari akamjibu, “Namkimbia bimkubwa wangu Sarai.” Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa bimkubwa wako Sarai na umtii.” Zaidi ya hayo, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Hagari, “Nitawazidisha wazawa wako hata wasiweze kuhesabika kwa wingi wao.” Kisha huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe ni mjamzito na utajifungua mtoto wa kiume; utamwita Ishmaeli, maana Mwenyezi-Mungu amesikia mateso yako. Ishmaeli ataishi kama pundamwitu; atakuwa adui wa kila mtu na kila mtu atakuwa adui yake. Ataishi akiwa adui wa jamaa yake.” Basi, Hagari akampa jina Mwenyezi-Mungu aliyezungumza naye huko, “Wewe ni Mungu Aonaye” kwa maana alifikiri, “Kweli hapa nimemwona yeye anionaye!” Ndiyo maana kile kisima chaitwa Beer-lahai-roi. Kisima hiki kipo kati ya Kadeshi na Beredi. Hagari akamzalia Abramu mtoto wa kiume. Abramu akamwita mtoto huyo Ishmaeli. Abramu alikuwa na umri wa miaka 86 wakati Hagari alipomzaa Ishmaeli.

Soma Mwanzo 16