Mwanzo 16:7-16
Mwanzo 16:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamkuta Hagari penye chemchemi ya maji jangwani, chemchemi iliyoko njiani kuelekea Shuri. Malaika akamwuliza, “Hagari, mjakazi wa Sarai! Unatoka wapi na unakwenda wapi?” Hagari akamjibu, “Namkimbia bimkubwa wangu Sarai.” Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa bimkubwa wako Sarai na umtii.” Zaidi ya hayo, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Hagari, “Nitawazidisha wazawa wako hata wasiweze kuhesabika kwa wingi wao.” Kisha huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe ni mjamzito na utajifungua mtoto wa kiume; utamwita Ishmaeli, maana Mwenyezi-Mungu amesikia mateso yako. Ishmaeli ataishi kama pundamwitu; atakuwa adui wa kila mtu na kila mtu atakuwa adui yake. Ataishi akiwa adui wa jamaa yake.” Basi, Hagari akampa jina Mwenyezi-Mungu aliyezungumza naye huko, “Wewe ni Mungu Aonaye” kwa maana alifikiri, “Kweli hapa nimemwona yeye anionaye!” Ndiyo maana kile kisima chaitwa Beer-lahai-roi. Kisima hiki kipo kati ya Kadeshi na Beredi. Hagari akamzalia Abramu mtoto wa kiume. Abramu akamwita mtoto huyo Ishmaeli. Abramu alikuwa na umri wa miaka 86 wakati Hagari alipomzaa Ishmaeli.
Mwanzo 16:7-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, na unakwenda wapi? Akanena, Namkimbia bimkubwa wangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bimkubwa wako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama punda mwitu kati ya watu, mkono wake utapingana na watu wote na mkono wa kila mtu ukipingana naye; na ataishi kwa ugomvi na jamaa yake yote. Akampa jina BWANA aliyesema naye, “Wewe U Mungu uonaye,” kwani alisema, “Kweli nimemwona Mungu na nikaendelea kuishi baada ya kumuona?” Kwa hiyo kisima kile kiliitwa Beer-lahai-roi. Tazama, kiko kati ya Kadeshi na Beredi. Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume; Abramu akamwita jina lake Ishmaeli, yule mwanawe, ambaye Hajiri alimzaa. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajiri alipomzalia Abramu Ishmaeli.
Mwanzo 16:7-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. Akaliita jina la BWANA aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona yeye anionaye? Kwa hiyo kisima kile kiliitwa Beer-lahai-roi. Tazama, kiko kati ya Kadeshi na Beredi. Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume; Abramu akamwita jina lake Ishmaeli, yule mwanawe, ambaye Hajiri alimzaa. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajiri alipomzalia Abramu Ishmaeli.
Mwanzo 16:7-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Malaika wa Mwenyezi Mungu akamkuta Hajiri karibu na chemchemi huko jangwani; chemchemi hiyo ilikuwa kando ya barabara iendayo Shuri. Malaika akamwambia, “Hajiri, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi, na unaenda wapi?” Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.” Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.” Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.” Pia malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia: “Wewe sasa una mimba nawe utamzaa mwana. Utamwita jina lake Ishmaeli, kwa sababu Mwenyezi Mungu amesikia kuhusu huzuni yako. Atakuwa kama punda-mwitu kati ya wanadamu; mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu, na mkono wa kila mtu utakuwa dhidi yake, naye ataishi kwa uhasama na ndugu zake wote.” Hajiri akampa Mwenyezi Mungu aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.” Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi; bado kipo hata leo kati ya Kadeshi na Beredi. Hivyo Hajiri akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hajiri aliyemzalia jina la Ishmaeli. Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita Hajiri alipomzalia Ishmaeli.