Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 16:7-16

Mwanzo 16:7-16 NENO

Malaika wa Mwenyezi Mungu akamkuta Hajiri karibu na chemchemi huko jangwani; chemchemi hiyo ilikuwa kando ya barabara iendayo Shuri. Malaika akamwambia, “Hajiri, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi, na unaenda wapi?” Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.” Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.” Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.” Pia malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia: “Wewe sasa una mimba nawe utamzaa mwana. Utamwita jina lake Ishmaeli, kwa sababu Mwenyezi Mungu amesikia kuhusu huzuni yako. Atakuwa kama punda-mwitu kati ya wanadamu; mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu, na mkono wa kila mtu utakuwa dhidi yake, naye ataishi kwa uhasama na ndugu zake wote.” Hajiri akampa Mwenyezi Mungu aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.” Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi; bado kipo hata leo kati ya Kadeshi na Beredi. Hivyo Hajiri akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hajiri aliyemzalia jina la Ishmaeli. Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita Hajiri alipomzalia Ishmaeli.