Mwanzo 16:7-16
Mwanzo 16:7-16 NEN
Malaika wa BWANA akamkuta Hagari karibu na chemchemi huko jangwani; ilikuwa chemchemi ile iliyokuwa kando ya barabara iendayo Shuri. Malaika akamwambia, “Hagari, mtumishi wa Sarai, umetokea wapi, na unakwenda wapi?” Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.” Ndipo malaika wa BWANA akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.” Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.” Pia malaika wa BWANA akamwambia: “Wewe sasa una mimba nawe utamzaa mwana. Utamwita jina lake Ishmaeli, kwa sababu BWANA amesikia juu ya huzuni yako. Atakuwa punda-mwitu katikati ya wanadamu, mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu na mkono wa kila mtu dhidi yake, naye ataishi kwa uhasama na ndugu zake wote.” Hagari akampa BWANA aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.” Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi, ambacho bado kipo huko hata leo kati ya Kadeshi na Beredi. Hivyo Hagari akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hagari aliyemzalia, Ishmaeli. Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita wakati Hagari alipomzalia Ishmaeli.