Wagalatia 6:11-18
Wagalatia 6:11-18 BHN
Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe. Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha nyinyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: Kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; huwataka nyinyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu. Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya. Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli – watu wa Mungu. Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu. Ndugu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amina.