Wagalatia 6:11-18
Wagalatia 6:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe. Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha nyinyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: Kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; huwataka nyinyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu. Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya. Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli – watu wa Mungu. Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu. Ndugu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amina.
Wagalatia 6:11-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tazameni niandikavyo kwa herufi kubwa niwaandikiapo kwa mkono wangu mimi mwenyewe! Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu. Lakini mimi, la hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutotahiriwa, ila kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
Wagalatia 6:11-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tazameni ni kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe! Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu. Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
Wagalatia 6:11-18 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Angalieni herufi kubwa ninazotumia nikiwaandikia kwa mkono wangu mwenyewe! Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Al-Masihi. Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. Lakini mimi naomba nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, ambaye kwake ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. Kwa maana katika Al-Masihi Isa, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, hata kwa Israeli wa Mungu. Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Isa. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe pamoja na roho zenu. Amen.