Ezekieli 40:28-47
Ezekieli 40:28-47 BHN
Yule mtu akanipitisha kwenye njia ya kuingilia upande wa kusini, tukafika kwenye ua wa ndani. Aliipima hiyo njia nayo ilikuwa sawa na zile njia nyingine za kuingilia kwenye kuta za nje. Vyumba vya walinzi, ukumbi, na kuta zake vilikuwa na ukubwa uleule kama vile vingine; kulikuwa na madirisha pia kandokando ya hiyo njia ya kuingilia na kwenye ukumbi. Ilikuwa na urefu mita 25 na upana mita kumi na mbili u nusu. Kulikuwa na vyumba kandokando ya hiyo njia ya kuingilia, vikiwa na urefu wa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Ule ukumbi ulikuwa mkabala na ua wa nje. Na kulikuwa na michoro ya mitende kwenye nguzo kandokando ya hiyo njia ya kuingilia kwenye ngazi. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia lango hili. Yule mtu alinipeleka upande wa mashariki wa ua wa ndani. Akaipima ile njia ya kuingilia, nayo ilikuwa na urefu kama zile njia nyingine za kuingilia. Vyumba vyake vya walinzi, nguzo zake za ndani pamoja na ukumbi vilikuwa na ukubwa kama vile vingine. Kulikuwa na madirisha pande zote hata kwenye matao na chumba cha kuingilia. Urefu wake ulikuwa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Kile chumba cha kuingilia kilikuwa mkabala na uwanja wa nje. Mitende ilichorwa kwenye kuta kwenye nafasi ya kupitia. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia kuelekea kwenye lango hili. Kisha yule mtu akanipeleka kwenye njia ya kuingilia upande wa kaskazini. Basi, akaipima hiyo njia ya kuingilia, nayo ilikuwa sawa na zile njia nyingine. Huko nako kulikuwa na vyumba vya walinzi, kuta za ndani zilizopambwa, ukumbi wa kuingilia na madirisha pande zote. Urefu wake wote ulikuwa mita 25 na upana mita kumi na mbili u nusu. Ule ukumbi wa kuingilia ulikuwa mkabala na ua wa nje; kulikuwa na mitende imechorwa kwenye kuta za hiyo nafasi ya kupitia. Pia kulikuwa na ngazi nane za kupandia kuelekea kwenye lango hili. Kwenye ua wa nje, kulikuwa na chumba cha ziada kilichounganishwa na njia ya kuingilia ya ndani, upande wa kaskazini. Chumba hicho kilikuwa mkabala na ukumbi wa kuingia, na huko walisafishia wanyama waliochinjwa kwa ajili ya tambiko za kuteketezwa nzima. Halafu katika ukumbi karibu na njia kulikuwako meza mbili upande mmoja na nyingine mbili upande mwingine. Meza hizo zilitumika kuwa mahali pa kuchinjia sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuondoa hatia. Nje ya ukumbi huo, kulikuwa na meza mbili upande mmoja na mbili upande mwingine wa njia ya kuingilia kwenye lango la kaskazini. Meza zote ambazo zilitumiwa kwa kuchinjia wanyama wa tambiko zilikuwa nane: Meza nne ndani ya ukumbi na meza nne nje ya ukumbi. Kulikuwako pia meza nne ndani ya ukumbi zilizotumiwa kuandalia sadaka za kuteketezwa. Meza hizo zilikuwa zimejengwa kwa mawe yaliyochongwa. Kimo cha kila meza kilikuwa sentimita 50 na upande wake wa juu ulikuwa mraba wenye upana wa sentimita 75. Vifaa vyote vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka nyingine viliwekwa juu ya meza hizo. Ndani ya ukumbi huo palizungukwa na vijiti vya kutundikia urefu wa kitanga, na nyama ziliwekwa mezani. Nje ya njia ya ndani kulikuwako vyumba vya walinzi kwenye ua wa ndani uliokuwa upande wa kaskazini wa njia. Vyumba hivyo vilielekea upande wa kusini. Chumba kimoja kilichokuwa upande wa lango la mashariki kilielekea upande wa kaskazini. Yule mtu akaniambia, “Chumba hiki kinachoelekea kusini ni kwa ajili ya makuhani wanaohudumu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na chumba kinachoelekea kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wanaohudumu madhabahuni. Makuhani hawa ni wale wa ukoo wa Sadoki, ndio hao kati ya watu wa kabila la Lawi wanaoruhusiwa kwenda mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Yule mtu akaupima ua wa ndani, nao ulikuwa mraba: Pande zote zilikuwa na upana wa mita 50. Madhabahu yalikuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.