Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 40:28-47

Ezekieli 40:28-47 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha akanileta mpaka ua wa ndani karibu na lango lililoelekea kusini; akalipima lango la kusini kwa vipimo vivyo hivyo; navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Tena palikuwa na matao pande zote, urefu wake dhiraa ishirini na tano na upana wake dhiraa tano. Na matao yake yaliuelekea ua wa nje, na mitende ilikuwa juu ya miimo yake; palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. Akanileta mpaka ua wa ndani ulioelekea upande wa mashariki, akalipima lango kwa vipimo vivyo hivyo; navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, kwa vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Na matao yake yaliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. Akanileta mpaka lango lililoelekea upande wa kaskazini; akalipima kwa vipimo vivyo hivyo; vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake; tena palikuwa na madirisha ndani yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Na miimo yake iliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. Na chumba, pamoja na lango lake, kilikuwa karibu na miimo ya malango; ndiko walikoiosha sadaka ya kuteketezwa. Na katika ukumbi wa lango palikuwa na meza mbili upande huu, na meza mbili upande huu, ili kuichinja sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia. Na upande mmoja, nje, penye madaraja ya kuliingia lango lililoelekea kaskazini, palikuwa na meza mbili; na upande wa pili, ulio wa ukumbi wa lango hilo, palikuwa na meza mbili. Palikuwa na meza nne upande huu, na meza nne upande huu, karibu na lango; meza nane ambazo juu yake walizichinja sadaka. Tena palikuwa na meza nne kwa sadaka za kuteketezwa, za mawe yaliyochongwa; urefu wake dhiraa moja na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja; juu yake waliviweka vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka. Tena hizo kulabu, ambazo urefu wake ni shubiri, zilifungwa ndani pande zote; na juu ya meza hizo ilikuwako nyama ya matoleo. Tena nje ya lango la ndani palikuwa na vyumba kwa waimbaji, katika ua wa ndani, uliokuwa kando ya lango lililoelekea kaskazini, navyo vilikabili upande wa kusini; na kimoja kando ya lango lililoelekea upande wa mashariki, kilikabili upande wa kaskazini. Akaniambia, Chumba hiki kinachokabili upande wa kusini ni kwa ajili ya makuhani, yaani, hao wasimamizi wa nyumba. Nacho chumba kinachokabili upande wa kaskazini ni cha makuhani, wasimamizi wa madhabahu; hao ni wana wa Sadoki, ambao kati ya wana wa Lawi, ndio waliomkaribia BWANA, ili kumtumikia. Akaupima huo ua, na urefu wake ulikuwa dhiraa mia moja, na upana wake dhiraa mia moja, mraba; nayo madhabahu yalikuwa mbele ya nyumba.

Ezekieli 40:28-47 Biblia Habari Njema (BHN)

Yule mtu akanipitisha kwenye njia ya kuingilia upande wa kusini, tukafika kwenye ua wa ndani. Aliipima hiyo njia nayo ilikuwa sawa na zile njia nyingine za kuingilia kwenye kuta za nje. Vyumba vya walinzi, ukumbi, na kuta zake vilikuwa na ukubwa uleule kama vile vingine; kulikuwa na madirisha pia kandokando ya hiyo njia ya kuingilia na kwenye ukumbi. Ilikuwa na urefu mita 25 na upana mita kumi na mbili u nusu. Kulikuwa na vyumba kandokando ya hiyo njia ya kuingilia, vikiwa na urefu wa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Ule ukumbi ulikuwa mkabala na ua wa nje. Na kulikuwa na michoro ya mitende kwenye nguzo kandokando ya hiyo njia ya kuingilia kwenye ngazi. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia lango hili. Yule mtu alinipeleka upande wa mashariki wa ua wa ndani. Akaipima ile njia ya kuingilia, nayo ilikuwa na urefu kama zile njia nyingine za kuingilia. Vyumba vyake vya walinzi, nguzo zake za ndani pamoja na ukumbi vilikuwa na ukubwa kama vile vingine. Kulikuwa na madirisha pande zote hata kwenye matao na chumba cha kuingilia. Urefu wake ulikuwa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Kile chumba cha kuingilia kilikuwa mkabala na uwanja wa nje. Mitende ilichorwa kwenye kuta kwenye nafasi ya kupitia. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia kuelekea kwenye lango hili. Kisha yule mtu akanipeleka kwenye njia ya kuingilia upande wa kaskazini. Basi, akaipima hiyo njia ya kuingilia, nayo ilikuwa sawa na zile njia nyingine. Huko nako kulikuwa na vyumba vya walinzi, kuta za ndani zilizopambwa, ukumbi wa kuingilia na madirisha pande zote. Urefu wake wote ulikuwa mita 25 na upana mita kumi na mbili u nusu. Ule ukumbi wa kuingilia ulikuwa mkabala na ua wa nje; kulikuwa na mitende imechorwa kwenye kuta za hiyo nafasi ya kupitia. Pia kulikuwa na ngazi nane za kupandia kuelekea kwenye lango hili. Kwenye ua wa nje, kulikuwa na chumba cha ziada kilichounganishwa na njia ya kuingilia ya ndani, upande wa kaskazini. Chumba hicho kilikuwa mkabala na ukumbi wa kuingia, na huko walisafishia wanyama waliochinjwa kwa ajili ya tambiko za kuteketezwa nzima. Halafu katika ukumbi karibu na njia kulikuwako meza mbili upande mmoja na nyingine mbili upande mwingine. Meza hizo zilitumika kuwa mahali pa kuchinjia sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuondoa hatia. Nje ya ukumbi huo, kulikuwa na meza mbili upande mmoja na mbili upande mwingine wa njia ya kuingilia kwenye lango la kaskazini. Meza zote ambazo zilitumiwa kwa kuchinjia wanyama wa tambiko zilikuwa nane: Meza nne ndani ya ukumbi na meza nne nje ya ukumbi. Kulikuwako pia meza nne ndani ya ukumbi zilizotumiwa kuandalia sadaka za kuteketezwa. Meza hizo zilikuwa zimejengwa kwa mawe yaliyochongwa. Kimo cha kila meza kilikuwa sentimita 50 na upande wake wa juu ulikuwa mraba wenye upana wa sentimita 75. Vifaa vyote vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka nyingine viliwekwa juu ya meza hizo. Ndani ya ukumbi huo palizungukwa na vijiti vya kutundikia urefu wa kitanga, na nyama ziliwekwa mezani. Nje ya njia ya ndani kulikuwako vyumba vya walinzi kwenye ua wa ndani uliokuwa upande wa kaskazini wa njia. Vyumba hivyo vilielekea upande wa kusini. Chumba kimoja kilichokuwa upande wa lango la mashariki kilielekea upande wa kaskazini. Yule mtu akaniambia, “Chumba hiki kinachoelekea kusini ni kwa ajili ya makuhani wanaohudumu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na chumba kinachoelekea kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wanaohudumu madhabahuni. Makuhani hawa ni wale wa ukoo wa Sadoki, ndio hao kati ya watu wa kabila la Lawi wanaoruhusiwa kwenda mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Yule mtu akaupima ua wa ndani, nao ulikuwa mraba: Pande zote zilikuwa na upana wa mita 50. Madhabahu yalikuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

Ezekieli 40:28-47 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha akanileta mpaka ua wa ndani karibu na lango lililoelekea kusini; akalipima lango la kusini kwa vipimo vivyo hivyo; navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Tena palikuwa na matao pande zote, urefu wake dhiraa ishirini na tano na upana wake dhiraa tano. Na matao yake yaliuelekea ua wa nje, na mitende ilikuwa juu ya miimo yake; palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. Akanileta mpaka ua wa ndani ulioelekea upande wa mashariki, akalipima lango kwa vipimo vivyo hivyo; navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, kwa vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Na matao yake yaliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. Akanileta mpaka lango lililoelekea upande wa kaskazini; akalipima kwa vipimo vivyo hivyo; vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake; tena palikuwa na madirisha ndani yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Na miimo yake iliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia. Na chumba, pamoja na lango lake, kilikuwa karibu na miimo ya malango; ndiko walikoiosha sadaka ya kuteketezwa. Na katika ukumbi wa lango palikuwa na meza mbili upande huu, na meza mbili upande huu, ili kuichinja sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia. Na upande mmoja, nje, penye madaraja ya kuliingia lango lililoelekea kaskazini, palikuwa na meza mbili; na upande wa pili, ulio wa ukumbi wa lango hilo, palikuwa na meza mbili. Palikuwa na meza nne upande huu, na meza nne upande huu, karibu na lango; meza nane ambazo juu yake walizichinja sadaka. Tena palikuwa na meza nne kwa sadaka za kuteketezwa, za mawe yaliyochongwa; urefu wake dhiraa moja na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja; juu yake waliviweka vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka. Tena hizo kulabu, ambazo urefu wake ni shubiri, zilifungwa ndani pande zote; na juu ya meza hizo ilikuwako nyama ya matoleo. Tena nje ya lango la ndani palikuwa na vyumba kwa waimbaji, katika ua wa ndani, uliokuwa kando ya lango lililoelekea kaskazini, navyo vilikabili upande wa kusini; na kimoja kando ya lango lililoelekea upande wa mashariki, kilikabili upande wa kaskazini. Akaniambia, Chumba hiki kinachokabili upande wa kusini ni kwa makuhani, yaani, hao walinzi wa malindo ya nyumba. Nacho chumba kinachokabili upande wa kaskazini ni kwa makuhani, walinzi wa malindo ya madhabahu; hao ni wana wa Sadoki, ambao miongoni mwa wana wa Lawi wamkaribia BWANA, ili kumtumikia. Akaupima huo ua, na urefu wake ulikuwa dhiraa mia, na upana wake dhiraa mia, mraba; nayo dhabahu ilikuwa mbele ya nyumba.

Ezekieli 40:28-47 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha akanileta mpaka ukumbi wa ndani kwa kupitia lango la kusini, naye akapima lango la kusini, ambalo lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine. Vyumba vyake, kuta zilizogawanya vyumba na ukumbi wake zilikuwa na vipimo sawasawa na zile nyingine. Hilo lango na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Navyo vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano. (Baraza za malango zilizozunguka ukumbi wa ndani zilikuwa na upana wa dhiraa ishirini na tano na kina cha dhiraa tano.) Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko. Kisha akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani ulioko upande wa mashariki, naye akalipima lango hilo, lilikuwa na vipimo vilivyo sawasawa na yale mengine. Vyumba vyake, kuta zake na baraza yake vilikuwa na vipimo vilivyo sawa na vile vingine. Lile lango pamoja na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Urefu wake ulikuwa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. Baraza yake ilielekea ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko. Kisha akanileta mpaka kwenye lango la kaskazini na kulipima. Lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine, kama vile ilivyokuwa kwa vyumba, kuta zake na baraza yake, tena kulikuwa na madirisha pande zote. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko. Kulikuwa na chumba na mlango karibu na baraza katika kila njia ya ndani ya lango ambamo sadaka za kuteketezwa zilioshwa. Kwenye baraza ya lile lango kulikuwepo meza mbili kila upande, ambako sadaka za kuteketezwa, sadaka za dhambi na sadaka za hatia zilichinjiwa. Karibu na ukuta wa nje wa baraza ya lile lango karibu na ngazi kwenye ingilio kuelekea kaskazini kulikuwa na meza mbili, nako upande mwingine wa ngazi kulikuwepo na meza mbili. Kwa hiyo kulikuwa na meza nne upande mmoja wa lango na nyingine nne upande mwingine, zote zilikuwa meza nane, ambapo dhabihu zilichinjiwa. Pia kulikuwa na meza nne za mawe yaliyochongwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, kila meza ilikuwa na urefu wa dhiraa moja na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu na kimo cha dhiraa moja. Juu ya meza hizo viliwekwa vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na dhabihu nyingine mbalimbali. Kulikuwa na kulabu, urefu wake nyanda nne, zilikuwa zimeshikizwa ukutani pande zote. Meza zilikuwa kwa ajili ya nyama za sadaka. Nje ya lango la ndani, kwenye ukumbi wa ndani, kulikuwa na vyumba viwili, kimoja upande wa lango la kaskazini nacho kilielekea kusini, kingine upande wa lango la kusini nacho kilielekea kaskazini. Akaniambia, “Chumba kinachoelekea upande wa kusini ni kwa ajili ya makuhani ambao wana usimamizi wa hekaluni, nacho chumba kinachoelekea upande wa kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wenye usimamizi wa madhabahuni. Hawa ni wana wa Sadoki, ambao ndio Walawi pekee wanaoweza kumkaribia BWANA ili kuhudumu mbele zake.” Ndipo alipopima ukumbi: nao ulikuwa mraba wa dhiraa mia moja urefu na upana. Madhabahu yalikuwa mbele ya Hekalu.