Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 40:28-47

Ezekieli 40:28-47 NEN

Kisha akanileta mpaka ukumbi wa ndani kwa kupitia lango la kusini, naye akapima lango la kusini, ambalo lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine. Vyumba vyake, kuta zilizogawanya vyumba na ukumbi wake zilikuwa na vipimo sawasawa na zile nyingine. Hilo lango na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Navyo vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano. (Baraza za malango zilizozunguka ukumbi wa ndani zilikuwa na upana wa dhiraa ishirini na tano na kina cha dhiraa tano.) Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko. Kisha akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani ulioko upande wa mashariki, naye akalipima lango hilo, lilikuwa na vipimo vilivyo sawasawa na yale mengine. Vyumba vyake, kuta zake na baraza yake vilikuwa na vipimo vilivyo sawa na vile vingine. Lile lango pamoja na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Urefu wake ulikuwa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. Baraza yake ilielekea ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko. Kisha akanileta mpaka kwenye lango la kaskazini na kulipima. Lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine, kama vile ilivyokuwa kwa vyumba, kuta zake na baraza yake, tena kulikuwa na madirisha pande zote. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko. Kulikuwa na chumba na mlango karibu na baraza katika kila njia ya ndani ya lango ambamo sadaka za kuteketezwa zilioshwa. Kwenye baraza ya lile lango kulikuwepo meza mbili kila upande, ambako sadaka za kuteketezwa, sadaka za dhambi na sadaka za hatia zilichinjiwa. Karibu na ukuta wa nje wa baraza ya lile lango karibu na ngazi kwenye ingilio kuelekea kaskazini kulikuwa na meza mbili, nako upande mwingine wa ngazi kulikuwepo na meza mbili. Kwa hiyo kulikuwa na meza nne upande mmoja wa lango na nyingine nne upande mwingine, zote zilikuwa meza nane, ambapo dhabihu zilichinjiwa. Pia kulikuwa na meza nne za mawe yaliyochongwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, kila meza ilikuwa na urefu wa dhiraa moja na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu na kimo cha dhiraa moja. Juu ya meza hizo viliwekwa vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na dhabihu nyingine mbalimbali. Kulikuwa na kulabu, urefu wake nyanda nne, zilikuwa zimeshikizwa ukutani pande zote. Meza zilikuwa kwa ajili ya nyama za sadaka. Nje ya lango la ndani, kwenye ukumbi wa ndani, kulikuwa na vyumba viwili, kimoja upande wa lango la kaskazini nacho kilielekea kusini, kingine upande wa lango la kusini nacho kilielekea kaskazini. Akaniambia, “Chumba kinachoelekea upande wa kusini ni kwa ajili ya makuhani ambao wana usimamizi wa hekaluni, nacho chumba kinachoelekea upande wa kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wenye usimamizi wa madhabahuni. Hawa ni wana wa Sadoki, ambao ndio Walawi pekee wanaoweza kumkaribia BWANA ili kuhudumu mbele zake.” Ndipo alipopima ukumbi: nao ulikuwa mraba wa dhiraa mia moja urefu na upana. Madhabahu yalikuwa mbele ya Hekalu.