Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 30:1-19

Ezekieli 30:1-19 BHN

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Toa unabii useme kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ombolezeni na kusema: ‘Ole wetu siku ile!’ Kwa maana, siku hiyo imekaribia; siku ile ya Mwenyezi-Mungu iko karibu. Hiyo itakuwa siku ya mawingu, siku ya maangamizi kwa mataifa. Vita vitazuka dhidi ya Misri, na wasiwasi mkuu utaikumba nchi ya Kushi, wakati Wamisri wengi wataanguka wameuawa, mali zao zitakapochukuliwa, na misingi ya miji yao kubomolewa. “Watu wote waliofungamana na Wamisri, yaani watu wa Kushi, Puti, Ludi, Arabia yote na Libia wataangamia pamoja nao. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wanaoiunga mkono Misri wataangamia, mashujaa wake wenye fahari wataangamizwa, tangu Migdoli mpaka Syene watu watauawa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Misri itakuwa jangwa kama nchi zilizo jangwa na miji yake itakuwa magofu kama miji iliyoteketezwa. Nitakapoiteketeza Misri kwa moto na kuwavunjilia mbali wasaidizi wake wote ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Siku hiyo, nitapeleka wajumbe kwenda kuwatisha Waethiopia wanaojidhani kuwa salama. Watatetemeka siku Misri itakapoangamia. Naam! Kweli siku hiyo yaja! “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitamtumia Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, kukomesha utajiri wa nchi ya Misri. Nebukadneza mwenyewe pamoja na watu wake, taifa katili kuliko mataifa yote, watatumwa kuiangamiza nchi ya Misri. Watachomoa panga zao dhidi ya Misri na kuijaza nchi hiyo watu waliouawa. Nitaukausha mto Nili na vijito vyake, na kuwauzia watu waovu nchi ya Misri. Nitasababisha uharibifu nchini kote kwa mkono wa watu wageni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaharibu vinyago vya miungu, na kukomesha sanamu mjini Memfisi. Hakutakuwa na mkuu tena huko Misri. Nitasababisha hofu itawale nchini Misri. Mji wa Pathrosi nitaufanya kuwa mtupu, mji wa Soani nitauwasha moto, mji wa Thebesi nitauadhibu. Nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu, ile ngome inayotegemewa na Misri; na kuangamiza makundi ya Thebesi. Nitaiwasha moto nchi ya Misri. Pelusiumu utashikwa na dhiki kubwa, ukuta wa Thebesi utabomolewa, nao Memfisi utakabiliwa na adui mchana wazi. Vijana wanaume wa Oni na Pi-besethi watauawa kwa upanga, na wakazi wengine watachukuliwa uhamishoni. Huko Tahpanesi mchana utakuwa giza wakati nitavunja mamlaka ya Misri na kiburi chake kikuu kukomeshwa. Wingu litaifunika nchi ya Misri na watu wake watachukuliwa mateka. Ndivyo nitakavyoiadhibu Misri. Na watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha