Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 30:1-19

Ezekieli 30:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Toa unabii useme kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ombolezeni na kusema: ‘Ole wetu siku ile!’ Kwa maana, siku hiyo imekaribia; siku ile ya Mwenyezi-Mungu iko karibu. Hiyo itakuwa siku ya mawingu, siku ya maangamizi kwa mataifa. Vita vitazuka dhidi ya Misri, na wasiwasi mkuu utaikumba nchi ya Kushi, wakati Wamisri wengi wataanguka wameuawa, mali zao zitakapochukuliwa, na misingi ya miji yao kubomolewa. “Watu wote waliofungamana na Wamisri, yaani watu wa Kushi, Puti, Ludi, Arabia yote na Libia wataangamia pamoja nao. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wanaoiunga mkono Misri wataangamia, mashujaa wake wenye fahari wataangamizwa, tangu Migdoli mpaka Syene watu watauawa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Misri itakuwa jangwa kama nchi zilizo jangwa na miji yake itakuwa magofu kama miji iliyoteketezwa. Nitakapoiteketeza Misri kwa moto na kuwavunjilia mbali wasaidizi wake wote ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Siku hiyo, nitapeleka wajumbe kwenda kuwatisha Waethiopia wanaojidhani kuwa salama. Watatetemeka siku Misri itakapoangamia. Naam! Kweli siku hiyo yaja! “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitamtumia Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, kukomesha utajiri wa nchi ya Misri. Nebukadneza mwenyewe pamoja na watu wake, taifa katili kuliko mataifa yote, watatumwa kuiangamiza nchi ya Misri. Watachomoa panga zao dhidi ya Misri na kuijaza nchi hiyo watu waliouawa. Nitaukausha mto Nili na vijito vyake, na kuwauzia watu waovu nchi ya Misri. Nitasababisha uharibifu nchini kote kwa mkono wa watu wageni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaharibu vinyago vya miungu, na kukomesha sanamu mjini Memfisi. Hakutakuwa na mkuu tena huko Misri. Nitasababisha hofu itawale nchini Misri. Mji wa Pathrosi nitaufanya kuwa mtupu, mji wa Soani nitauwasha moto, mji wa Thebesi nitauadhibu. Nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu, ile ngome inayotegemewa na Misri; na kuangamiza makundi ya Thebesi. Nitaiwasha moto nchi ya Misri. Pelusiumu utashikwa na dhiki kubwa, ukuta wa Thebesi utabomolewa, nao Memfisi utakabiliwa na adui mchana wazi. Vijana wanaume wa Oni na Pi-besethi watauawa kwa upanga, na wakazi wengine watachukuliwa uhamishoni. Huko Tahpanesi mchana utakuwa giza wakati nitavunja mamlaka ya Misri na kiburi chake kikuu kukomeshwa. Wingu litaifunika nchi ya Misri na watu wake watachukuliwa mateka. Ndivyo nitakavyoiadhibu Misri. Na watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Ezekieli 30:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Pigeni makelele ya uchungu, Ole wa siku ile! Kwa maana siku ile i karibu, siku ile ya BWANA i karibu, siku ya mawingu; itakuwa wakati wa maangamizi kwa mataifa. Na upanga utakuja juu ya Misri, na dhiki itakuwa katika Kushi, watakapoanguka watu waliouawa katika Misri, nao watauondoa wingi wa watu wake, na misingi yake itabomolewa. Kushi, na Putu, na Ludi, na watu wote waliochanganyika, na Kubu, na wana wa nchi ya agano, wataanguka kwa upanga pamoja nao. BWANA asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema Bwana MUNGU. Nao watakuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake itakuwamo kati ya miji iliyoharibika. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote wamsaidiao watakapoangamia. Katika siku hiyo watatoka wajumbe mbele zangu katika merikebu, ili kuwatia hofu Wakushi, wanaojiona kuwa salama, na dhiki itakuwa juu yao, vile vile kama katika siku ya Misri; kwa maana, tazama, inakuja. Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaukomesha wingi wa watu wa Misri, kwa mkono wa Nebukadneza, mfalme wa Babeli. Yeye, na watu wake pamoja naye, watu wa mataifa watishao, wataletwa waingie katika nchi waiharibu, nao watafuta panga zao wapigane na Misri, na kuijaza nchi wale waliouawa. Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya; nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni; mimi, BWANA, nimenena neno hili. Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili katika Nofu, wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika nchi ya Misri, nami nitatia hofu katika nchi ya Misri. Nami nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa, nami nitatia moto katika Soani, nami nitatekeleza hukumu katika No. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Sini, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali wingi wa watu wa No. Nami nitatia moto katika Misri; Sini itakuwa katika dhiki kuu, na No itavunjika kabisa; na Nofu itakuwa na adui wakati wa mchana. Vijana wa Oni, na wa Pi-besethi, wataanguka kwa upanga; na miji hiyo itakwenda utumwani. Huko Tapanesi nako mchana utakuwa giza, nitakapovunja huko kongwa za Misri, na kiburi cha uwezo wake kitakoma ndani yake, na katika habari zake, wingu litaifunika, na binti zake watakwenda utumwani. Hivyo ndivyo nitakavyotekeleza hukumu katika Misri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Ezekieli 30:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Pigeni makelele ya uchungu, Ole wa siku ile! Kwa maana siku ile i karibu, siku ile ya BWANA i karibu, siku ya mawingu; itakuwa wakati wa mataifa. Na upanga utakuja juu ya Misri, na dhiki itakuwa katika Kushi, watakapoanguka watu waliouawa katika Misri, nao watauondoa wingi wa watu wake, na misingi yake itabomolewa. Kushi, na Putu, na Ludi, na watu wote waliochanganyika, na Kubu, na wana wa nchi ya agano, wataanguka kwa upanga pamoja nao. BWANA asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema Bwana MUNGU. Nao watakuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake itakuwamo kati ya miji iliyoharibika. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote wamsaidiao watakapoangamia. Katika siku hiyo watatoka wajumbe mbele zangu katika merikebu, ili kuwatia hofu Wakushi, wanaojiona kuwa salama, na dhiki itakuwa juu yao, vile vile kama katika siku ya Misri; kwa maana, tazama, inakuja. Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaukomesha wingi wa watu wa Misri, kwa mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli. Yeye, na watu wake pamoja naye, watu wa mataifa watishao, wataletwa waingie katika nchi waiharibu, nao watafuta panga zao wapigane na Misri, na kuijaza nchi wale waliouawa. Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya; nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni; mimi, BWANA, nimenena neno hili. Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili katika Nofu, wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika nchi ya Misri, nami nitatia hofu katika nchi ya Misri. Nami nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa, nami nitatia moto katika Soani, nami nitatekeleza hukumu katika No. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Sini, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali wingi wa watu wa No. Nami nitatia moto katika Misri; Sini itakuwa katika dhiki kuu, na No itavunjika kabisa; na Nofu itakuwa na adui wakati wa mchana. Vijana wa Oni, na wa Pi-besethi, wataanguka kwa upanga; na miji hiyo itakwenda utumwani. Huko Tapanesi nako mchana utakuwa giza, nitakapovunja huko kongwa za Misri, na kiburi cha uwezo wake kitakoma ndani yake, na katika habari zake, wingu litaifunika, na binti zake watakwenda utumwani. Hivyo ndivyo nitakavyotekeleza hukumu katika Misri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Ezekieli 30:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, toa unabii na useme: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Ombolezeni ninyi na mseme, “Ole wa siku ile!” Kwa kuwa siku ile imekaribia, siku ya BWANA imekaribia, siku ya mawingu, siku ya maangamizi kwa mataifa. Upanga utakuja dhidi ya Misri, nayo maumivu makuu yataijia Ethiopia. Mauaji yatakapoangukia Misri, utajiri wake utachukuliwa na misingi yake itabomolewa. Kushi na Putu, Ludi na Arabia yote, Libya na watu wa nchi ya Agano watauawa kwa upanga pamoja na Misri. “ ‘Hili ndilo BWANA asemalo: “ ‘Wale walioungana na Misri wataanguka na kiburi cha nguvu zake kitashindwa. Kutoka Migdoli hadi Aswani, watauawa ndani yake kwa upanga, asema BWANA Mwenyezi. “ ‘Hizo nchi zitakua ukiwa miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yao itakuwa magofu miongoni mwa miji iliyo magofu. Ndipo watakapojua kwamba mimi ndimi BWANA, nitakapoiwasha Misri moto na wote wamsaidiao watapondwa. “ ‘Siku hiyo wajumbe watatoka kwangu kwa merikebu, ili kuwatia hofu Ethiopia, wakiwa katika hali yao ya kuridhika. Maumivu makali yatawapata siku ya maangamizi ya Misri, kwa kuwa hakika itakuja. “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Nitakomesha makundi ya wajeuri ya Misri kwa mkono wa Nebukadneza mfalme wa Babeli. Yeye na jeshi lake, taifa lililo katili kuliko mataifa yote, litaletwa ili kuangamiza nchi. Watafuta panga zao dhidi ya Misri na kuijaza nchi kwa waliouawa. Nitakausha vijito vya Naili na nitaiuza nchi kwa watu waovu, kwa mkono wa wageni, nitaifanya nchi ukiwa na kila kitu kilichomo ndani yake. Mimi BWANA nimenena haya. “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Nitaangamiza sanamu na kukomesha vinyago katika Memfisi Hapatakuwepo tena na mkuu katika nchi ya Misri, nami nitaeneza hofu katika nchi nzima. Nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa na kuitia moto Soani, nami nitaipiga kwa adhabu Thebesi Nitaimwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali makundi ya wajeuri wa Thebesi. Nitaitia moto nchi ya Misri; Pelusiumu itagaagaa kwa maumivu makuu. Thebesi itachukuliwa na tufani, Memfisi itakuwa katika taabu daima. Wanaume vijana wa Oni na wa Pi-Besethi wataanguka kwa upanga nayo hiyo miji itatekwa. Huko Tahpanhesi mchana utatiwa giza nitakapovunja kongwa la Misri; hapo kiburi cha nguvu zake kitakoma. Atafunikwa na mawingu na vijiji vyake vitatekwa. Kwa hiyo nitaipiga Misri kwa adhabu, nao watajua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”