Ezekieli 16:1-14
Ezekieli 16:1-14 BHN
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, ujulishe mji wa Yerusalemu machukizo yake. Uuambie kuwa, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nauambia Yerusalemu: Kwa asili wewe ulizaliwa katika nchi ya Kanaani. Baba yako alikuwa Mwamori, na mama yako alikuwa Mhiti. Siku ile ulipozaliwa, kitovu chako hakikukatwa wala hukuoshwa kwa maji; hukusuguliwa kwa chumvi wala hukuvishwa nguo za kitoto. Hakuna aliyekuonea huruma na kukufanyia mambo hayo. Hakuna aliyekupenda. Bali, siku ile ulipozaliwa, ulitupwa huko mashambani kwa sababu siku ulipozaliwa ulichukiza sana. “Mimi nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nilikuambia, ‘Ishi, na ukue kama mmea shambani.’ Nawe ukakua na kurefuka hata ukawa msichana. Matiti yako yakakua na nywele zako nazo zikakua. Lakini ulikuwa uchi kabisa. “Nilipopita tena karibu nawe, nikakuona. Wakati huu, ulikuwa umefikia umri wa kupendwa kama msichana. Nikalitandaza vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikafanya nawe agano la ndoa, nawe ukawa wangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Kisha nikachukua maji, nikakuosha damu uliyokuwa nayo, nikakupaka mafuta. Nilikuvika pia vazi lililonakshiwa na viatu vya ngozi. Nikakuzungushia kitambaa cha kitani safi na mtandio wa hariri. Nikakupamba kwa vito, nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni. Nikakutia hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na kichwani mwako nikakupamba kwa taji nzuri. Basi, ukapambika kwa dhahabu na fedha. Vazi lako likawa la kitani safi na hariri, nalo lilikuwa limenakshiwa. Ulitumia unga safi, asali na mafuta kwa chakula chako. Ukawa mzuri kupindukia, ukaifikia hali ya kifalme. Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kutokana na uzuri wako, kwani uzuri wako ulikamilika kwa sababu ya fahari niliyokujalia. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.