Ezekieli 16:1-14
Ezekieli 16:1-14 SRUV
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, uujulishe Yerusalemu machukizo yake, useme, Bwana MUNGU auambia Yerusalemu hivi; Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani; Mwamori alikuwa baba yako, na mama yako alikuwa Mhiti. Na kuhusu habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa. Hakuna jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lolote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa. Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nilikuambia, Ulipokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nilikuambia, Ulipokuwa katika damu yako, uwe hai. Nilikufanya kuwa maelfu, kama mimea ya mashamba, ukaongezeka, na kuzidi kuwa mkubwa, ukapata kuwa na uzuri mno; matiti yako yakaumbwa, nywele zako zikawa zimeota; lakini ulikuwa uchi, bila mavazi. Basi, nilipopita karibu nawe, nikakutazama; tazama, wakati wako ulikuwa wakati wa upendo; nikatandika upindo wa vazi langu juu yako, nikakufunika uchi wako; naam, nilikuapia, nikafanya agano nawe, asema Bwana MUNGU, ukawa wangu. Kisha nikakuosha kwa maji; naam, nilikuosha kabisa damu yako, na kukupaka mafuta; nikakuvika nguo ya taraza, nikakupa viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nguo ya kitani safi kiunoni mwako, nikakufunika kwa hariri. Nikakupamba kwa mapambo pia, nikatia vikuku mikononi mwako, na mkufu shingoni mwako. Nikatia kishaufu puani mwako, na herini masikioni mwako, na taji zuri juu ya kichwa chako. Hivyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; na mavazi yako yalikuwa ya kitani safi, na hariri, na kazi ya taraza; ulikula unga mzuri, na asali, na mafuta; nawe ulikuwa mzuri mno, ukafanikiwa hata kufikia hali ya kifalme. Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia, asema Bwana MUNGU.