Ezekieli 16:1-14
Ezekieli 16:1-14 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, kabili Yerusalemu kuhusu matendo yake ya kuchukiza, useme, ‘Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi, analomwambia Yerusalemu: Asili na kuzaliwa kwako kulikuwa ni katika nchi ya Wakanaani; baba yako alikuwa Mwamori, naye mama yako alikuwa Mhiti. Siku uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuogeshwa kwa maji ili kukufanya safi, wala hukusuguliwa kwa chumvi wala kufunikwa kwa nguo. Hakuna yeyote aliyekuonea huruma au kukusikitikia kiasi cha kukutendea mojawapo ya mambo haya. Badala yake, ulipozaliwa ulitupwa nje penye uwanja, kwa kuwa katika siku uliyozaliwa ulidharauliwa. “ ‘Nami nikapita karibu nawe nikakuona ukigaagaa kwenye damu yako, nawe ulipokuwa umelala hapo penye hiyo damu nikakuambia, “Ishi!” Nilikufanya uote kama mmea wa shambani. Ukakua na kuongezeka sana, ukawa kito cha thamani kuliko vyote. Matiti yako yakatokeza na nywele zako zikaota, wewe uliyekuwa uchi na bila kitu chochote. “ ‘Baadaye nikapita karibu nawe, nilipokutazama na kukuona kuwa umefikia umri wa kupendwa, niliutandaza upindo wa vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikakuapia na kuingia kwenye agano na wewe, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nawe ukawa wangu. “ ‘Nilikuogesha kwa maji, nikakuosha ile damu na kukupaka mafuta. Nikakuvika vazi lililotariziwa na kukuvalisha viatu vya ngozi. Nikakuvika nguo za kitani safi na kukufunika kwa mavazi ya thamani kubwa. Nikakupamba kwa vito: nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni mwako, nikaweka hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na taji nzuri sana kichwani mwako. Kwa hiyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; nguo zako zilikuwa za kitani safi, na hariri, na nguo iliyokuwa imetariziwa. Chakula chako kilikuwa unga laini, asali na mafuta ya zeituni. Ukawa mzuri sana, ukainuka kuwa malkia. Umaarufu wako ulifahamika miongoni mwa mataifa kwa ajili ya uzuri wako, kwani ulikuwa mkamilifu kwa ajili ya utukufu wangu niliokuwa nimeuweka juu yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.