Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 35:20-29

Kutoka 35:20-29 BHN

Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikaondoka mbele ya Mose. Kila mtu aliyevutwa na kusukumwa moyoni mwake alimtolea Mungu mchango wake kwa ajili ya hema la mkutano, huduma zake zote na mavazi yake matakatifu. Hivyo wote wenye moyo mkarimu, wanaume kwa wanawake, wakaleta vipini, pete za mhuri, vikuku na kila aina ya vyombo vya dhahabu; kila mtu akamtolea Mwenyezi-Mungu kitu cha dhahabu. Kila mtu alileta chochote alichokuwa nacho kama vile sufu ya rangi ya buluu zambarau na nyekundu, au kitani safi, au manyoya ya mbuzi au ngozi ya kondoo iliyotiwa rangi nyekundu. Kila mtu aliyeweza kutoa fedha au shaba aliileta kwa Mwenyezi-Mungu kama toleo lake. Tena mtu yeyote aliyekuwa na mbao za mjohoro alileta pia. Wanawake wote waliokuwa na ujuzi wa kufuma walileta vitu walivyofuma kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Na wanawake wote waliokuwa na ujuzi walisokota manyoya ya mbuzi. Viongozi walileta vito vya rangi na mawe mengine kwa ajili ya kizibao na kifuko cha kifuani; walileta pia viungo na mafuta kwa ajili ya taa, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri. Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, ambao walivutwa moyoni mwao kuleta chochote kwa ajili ya kazi ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwagiza Mose ifanyike, walileta vitu hivyo kwa hiari, kama mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu.

Soma Kutoka 35