Kutoka 35:20-29
Kutoka 35:20-29 NEN
Ndipo jumuiya yote ya Waisraeli ilipoondoka mbele ya Mose, na kila mmoja aliyependa na ambaye moyo wake ulimsukuma alikuja na kuleta sadaka kwa BWANA, kwa ajili ya kazi katika Hema la Kukutania, kwa ajili ya huduma yake yote na kwa ajili ya mavazi matakatifu. Wote waliokuwa na utayari, wanaume kwa wanawake, wakaja wakaleta vito vya dhahabu vya kila aina: vipini, vipuli, pete na mapambo. Wote wakatoa dhahabu zao kama sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA. Kila mmoja aliyekuwa na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi, au singa za mbuzi, ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, au ngozi za pomboo, wakavileta. Wale waliotoa sadaka ya fedha au shaba wakavileta kama sadaka kwa BWANA, na kila aliyekuwa na mti wa mshita kwa ajili ya kazi yoyote ile akauleta. Kila mwanamke aliyekuwa na ujuzi alisokota kwa mikono yake na alileta kile alichosokota, iwe ni nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi. Wanawake wote waliopenda na waliokuwa na ujuzi wakasokota singa za mbuzi. Viongozi wakaleta vito vya shohamu pamoja na vito vingine vya thamani kwa ajili ya kuweka kwenye kisibau na kwenye kifuko cha kifuani. Wakaleta pia vikolezi na mafuta ya zeituni kwa ajili ya mwanga, kwa ajili ya mafuta ya upako na kwa ajili ya uvumba wenye harufu nzuri. Waisraeli wote waume kwa wake waliokuwa wanapenda wakaleta mbele za BWANA kwa hiari yao wenyewe sadaka kwa ajili ya kazi yote ya BWANA aliyokuwa amewaagiza kuifanya kupitia kwa Mose.