Kutoka 35:20-29
Kutoka 35:20-29 SRUV
Basi mkutano wote wa wana wa Israeli wakaondoka hapo mbele ya Musa. Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka za kumpa BWANA, kwa kazi ya hema ya kukutania, na kwa utumishi wake, na kwa hayo mavazi matakatifu. Nao wakaja, wanaume kwa wanawake, wote waliokuwa na moyo wa kupenda, wakaleta vipini, hazama, pete za mhuri, vikuku na vyombo vyote vya dhahabu; kila mtu aliyetoa toleo la dhahabu la kumpa BWANA. Tena kila mtu aliyeona kwake nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri, singa za mbuzi, ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu na ngozi za pomboo, akavileta. Kila mtu aliyetoa toleo la fedha, na la shaba, akaileta sadaka ya BWANA; na kila mtu, aliyeona kwake mti wa mshita kwa kazi yoyote ya huo utumishi, akauleta. Na wanawake wote waliokuwa na mioyo ya hekima, walisokota kwa mikono yao, nao wakaleta hizo walizokuwa wamezisokota, nguo za rangi ya samawati, na za rangi ya zambarau, na hizo nyuzi nyekundu, na hiyo nguo ya kitani nzuri. Na wanawake wote ambao mioyo yao iliwahimiza katika hekima wakasokota hizo singa za mbuzi. Na hao wakuu wakavileta vile vito vya shohamu, na vito vya kutiwa, kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani, na viungo vya manukato, na mafuta; kwa hiyo taa, na kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri. Wana wa Israeli wakaleta sadaka za kumpa BWANA kwa moyo wa kupenda; wote, wanaume kwa wanawake, ambao mioyo yao iliwafanya kuwa wapenda kuleta kwa hiyo kazi, ambayo BWANA aliamuru ifanywe kwa mkono wa Musa.